Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ametangaza kuwa Wizara yake itaendelea kutekeleza vipaumbele sita muhimu katika mwaka wa fedha 2026/2027, kwa lengo la kuimarisha sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni mjini Dodoma, Waziri Chongolo alisema vipaumbele hivyo ni pamoja na kuongeza tija na uzalishaji, kukuza ajira zenye staha hasa kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha upatikanaji wa mitaji, masoko na kuongeza mauzo ya mazao nje ya nchi, kuendeleza sekta ya ushirika, na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kukuza kilimo cha kisasa.

Ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa, Wizara imeandaa jumla ya mikakati 30 itakayotekelezwa katika maeneo mbalimbali. Katika kipaumbele cha kuongeza tija na uzalishaji, Chongolo alieleza kuwa hatua kadhaa zitachukuliwa, ikiwemo kuimarisha utafiti wa kilimo, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora na miche, pamoja na kutoa ruzuku ya pembejeo kama mbolea, mbegu na viuatilifu.

Mikakati mingine ni pamoja na kusajili wakulima na kurasimisha shughuli zao, kuboresha huduma za ugani, kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja, kupima afya ya udongo, na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, Wizara inapanga kuanzisha vituo maalum vitakavyotoa huduma za zana za kisasa za kilimo ili kuongeza ufanisi kwa wakulima na kuchochea uzalishaji wenye tija.

Hatua hizi zinatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, huku zikilenga pia kuongeza kipato kwa wakulima na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...