-Benki Yathibitisha faida ya Sh bilioni 206 robo ya kwanza 2026.

Na Ashura Mohamed, Arusha

Benki ya CRDB imeahidi kuendelea kulinda misingi bora iliyoiweka katika nafasi nzuri ya kifedha nchini, huku ikichukua hatua za kuongeza kasi ya ukuaji kwa kuunda vitengo maalum vya wataalamu kulenga sekta za kimkakati kama mafuta, gesi, kilimo na madini.

Akizungumza mkoani Arusha wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa benki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, alisema lengo ni kuhakikisha benki inatoa huduma zote kwa wakati, kwa urahisi na kwa gharama nafuu, huku ikiendelea kujali mteja.

“Tumeunda vitengo maalum ndani ya benki yetu vyenye wataalamu. Lengo ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika sekta hizo na kunasa fursa mpya zitakazojitokeza kwa uwekezaji. Tunachunguza nchi inapoelekea ili tushinde katika maeneo hayo,” alisema Dkt. Nsekela.

Aliongeza kuwa CRDB itaendelea kudumisha mtaji imara, ubora wa mikopo na nidhamu ya kibiashara, huku ikitafuta fursa mpya katika sekta mtambuka kulingana na mwelekeo wa uchumi wa nchi.

Dkt. Nsekela pia aliomba wanahisa kuwa miongoni mwa wateja wa kwanza wa benki yao kwa kutumia huduma mbalimbali za kibenki ili kuiwezesha CRDB kusonga mbele zaidi. Alishukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa miongozo na sera ambazo zimekuwa dira ya mafanikio ya benki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa CRDB, Fredrick Nshekanabo, alisema benki imepata faida ya shilingi bilioni 206 baada ya kodi katika robo ya kwanza ya 2026.

Alisema rasilimali za benki zimekua kwa asilimia 35 hadi kufikia shilingi trilioni 23.9, ikilinganishwa na shilingi trilioni 17.6 zilizorekodiwa katika robo ya kwanza ya 2025.

“Ukuaji huu umechangiwa hasa na ukuaji wa mikopo ambao umeongezeka kwa asilimia 34 hadi kufikia shilingi trilioni 14.7. Tunaona ukuaji huo katika mikopo midogo, ya kati na ya kilimo, ambazo ni sekta muhimu kwetu kimkakati,” alisisitiza Nshekanabo.

Aliongeza kuwa Amana pia zimekua kwa asilimia 36 hadi kufikia shilingi trilioni 16.3, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wateja kwa benki.
Mkurugenzi wa fedha wa benki ya CRBB Fredrick Nshekanabo akizungumza wakati wa mkutano mkuu
Mkurugenzi wa benki ya CRBB Dkt.Abdulmajid Nsekela akizungumza na Wanahisa Jijini Arusha

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...