Chama kikuu cha Ushirika Tandahimba Newala Limited (TANECU) kimesema mfumo wa stakabadhi za ghala umeleta mafanikio makubwa kwa wakulima wa korosho pamoja na jamii za Wilaya za Tandahimba na Newala kupitia ongezeko la ushindani wa soko, ajira na ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.
Akizungumza Mei 18, 2026 katika maonesho ya miaka 20 ya mfumo wa stakabadhi za ghala yanayofanyika Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Bodi wa TANECU, Karimu Hamisi Chipola amesema mfumo huo ulianza mwaka 2006 katika Mkoa wa Mtwara hususan kwenye zao la korosho ambapo mwanzoni wakulima hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mfumo huo.
Amesema Serikali ilitoa elimu kwa wakulima huku TANECU ikipewa dhamana ya kusimamia mfumo huo kwa wakulima wa zao la korosho katika maeneo yao jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa.
Chipola amesema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo wakulima walikuwa wanauza mazao yao kupitia soko huria bila kuwepo ushindani wala usimamizi mzuri wa bei jambo lililosababisha wakulima wengi kupata hasara.
Amesema baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi za ghala, wakulima wamekuwa na uhakika wa soko pamoja na bei nzuri za mazao yao kutokana na ushindani ulioongezeka katika biashara ya korosho.
Aidha amesema mfumo huo umechangia kuongeza ajira katika maeneo yao kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye maghala ikiwemo watunza maghala, vibarua wa kubeba magunia pamoja na shughuli ndogondogo za biashara zinazofanywa na wananchi.
“Mfumo huu umeleta tija kubwa kwa wakulima na jamii kwa ujumla kwani umeongeza ushindani wa soko na kutoa uhakika wa masoko ya mazao,” amesema Chipola.
Ameongeza kuwa mfumo huo pia umeimarisha vyama vya ushirika ambapo TANECU imeendelea kusimamia ukusanyaji wa tozo mbalimbali za wadau kupitia mfumo huo.
Kwa mujibu wa Chipola, zaidi ya Shilingi Bilioni 6 zimekusanywa na Halmashauri kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala jambo lililosaidia kuongeza mapato ya Serikali za Mitaa.
Pia amesema TANECU imefanikiwa kujenga kiwanda cha kubangua korosho chenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.6 ambacho kwa sasa kinatoa ajira kwa zaidi ya wananchi 300.
Amesema chama hicho kinaendelea na hatua za mwisho za kujenga kiwanda kingine Wilaya ya Tandahimba kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao na kuwapa wakulima ushindani zaidi kwenye soko.
Aidha amesema TANECU kwa sasa ina maghala manne na ipo kwenye mkakati wa kujenga maghala sita zaidi ili kuimarisha uhifadhi wa mazao na kuongeza ufanisi wa mfumo wa stakabadhi za ghala katika maeneo yao.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...