Wafugaji nchini wameendelea kunufaika na huduma za kifedha baada ya kuongezeka kwa uelewa wao kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji, hatua iliyowezesha kurahisishwa kwa vigezo vya dhamana ya kupata mikopo kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Mifugo Kanda ya Ziwa, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Anselem Mwenda, amesema benki hiyo imefanikiwa kuwasaidia wafugaji wengi kupata mikopo kwa urahisi kupitia huduma mbalimbali ikiwemo bima ya mifugo.
Mwenda alitoa kauli hiyo mara baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, kutembelea banda la CRDB, ambao ni wadhamini wakuu wa maonyesho hayo.
Alisema kuwa kwa sasa wafugaji wana uwezo wa kukopesheka kwa urahisi zaidi kutokana na kuwa na bima ya mifugo pamoja na kutambuliwa kwa rasilimali zao kama sehemu ya dhamana.
“Uelewa wa wafugaji umeongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na ilivyokuwa zamani. Hii imewasaidia kutumia fursa za kifedha zinazotolewa na benki kwa maendeleo ya shughuli zao."
Aliongeza kuwa huduma zote za kibenki zinaendelea kutolewa katika banda la CRDB kwa kipindi cha siku mbili za maonyesho hayo, kuanzia Mei 30 hadi 31, huku akiwakaribisha wafugaji na wadau wengine kufika kupata huduma pamoja na elimu ya masuala ya fedha.
Mwenda alisisitiza umuhimu wa wafugaji kuendelea kujifunza kuhusu usimamizi wa fedha na matumizi sahihi ya mikopo ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...