Na Pamela Mollel,Arusha 

Jiji la Arusha linaendelea kushuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii pamoja na kuimarisha miundombinu katika maeneo tofauti ya jiji hilo. 

Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Arusha linaendelea kuwa moja ya majiji muhimu nchini katika sekta ya utalii na shughuli za kikanda.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranqhe, amesema katika kipindi cha robo ya tatu hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri imeendelea kutekeleza miradi yenye thamani ya mabilioni ya shilingi katika kata mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

Miongoni mwa miradi inayoendelea ni ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Moshono unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 145. Pia kuna ujenzi wa mtaro wa Suye wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100, mradi unaotarajiwa kusaidia kupunguza changamoto za miundombinu ya maji ya mvua katika eneo hilo.

Katika kuboresha mazingira na usimamizi wa taka, Halmashauri ya Jiji la Arusha inaendelea na ujenzi wa vifuko viwili vya kuhifadhi taka katika Kata ya Muriet kwa gharama inayozidi shilingi milioni 64.

 Sambamba na hilo, magari mawili mapya aina ya Toyota Pick Up yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 363 yamepokelewa ili kusaidia shughuli za utoaji wa huduma za kijamii.

Sekta ya elimu nayo imeendelea kupewa kipaumbele ambapo ujenzi wa Shule ya Sekondari Bondeni City unaendelea kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 760.

Aidha, ujenzi wa Shule ya Msingi Ungalimited nao unaendelea kwa zaidi ya shilingi milioni 877 ikiwa ni jitihada za kuongeza mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Meya Iranqhe amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha dhamira ya halmashauri katika kuimarisha maendeleo ya jiji pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na halmashauri katika kulinda na kuthamini miradi hiyo ili iweze kuleta manufaa ya muda mrefu kwa jamii na kuchochea maendeleo endelevu ya Jiji la Arusha.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...