Na mwandishi wetu
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amewataka waandishi wa habari pamoja na jamii kwa ujumla kutambua wajibu wao katika kusimamia malezi na makuzi ya watoto ili kujenga familia imara na taifa lenye maadili mema.
Akizungumza katika semina ya malezi iliyoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum Kairuki alisema mafanikio ya kibiashara, kiuongozi na kijamii hayawezi kuwa na maana endapo msingi wa familia katika malezi na makuzi haujajengwa vizuri.
“Tutambue hivyo, pamoja na yote utafanikiwa kibiashara, kiuongozi na mengine mengi lakini kama msingi wa familia yako katika malezi na makuzi haujakaa sawa utateteleka. Hata ukipata mafanikio yatakuwa ya muda mfupi na hutakuwa na faraja wala furaha, hivyo eneo hili ni la kusisitiza na kutilia mkazo,” alisema Kairuki.
Aidha, aliitaka jamii kuzingatia matumizi sahihi ya simu za mkononi pamoja na vyombo vingine vya teknolojia, akieleza kuwa watoto wengi wamejikuta wakitumia vibaya mitandao ya kijamii.
“Kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, laini ya simu hutolewa kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 kwenda juu. Sasa unabaki na maswali unapoambiwa watoto wetu wameona vitu vya hovyo, unajiuliza wanavionea wapi ilhali kanuni zinakataza,” alisema.
Kairuki alisisitiza kuwa mtoto hastahili kumiliki simu ya mkononi, huku akibainisha kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamelegeza usimamizi wao jambo linalochangia watoto kuathirika na matumizi mabaya ya teknolojia.
“Ni muhimu kwa wazazi kutambua kuwa sheria za nchi haziruhusu jambo hilo, hivyo niwaombe sana kutambua kuwa ulinzi unaanza na sisi wenyewe majumbani mwetu kwa kufuatilia watoto wetu wanaangalia nini chini ya ulinzi wetu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Kairuki alikemea tabia ya matusi, udhalilishaji na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisema vitendo hivyo ni kosa kisheria na vyombo vya dola vitaendelea kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kusimamia suala hili ikiwemo kufunga akaunti mbalimbali za watu watakaokiuka sheria. Mitandao ina fursa nyingi chanya kwa maendeleo binafsi na jamii hivyo itumike kwa manufaa,” alisema.
Naye Daktari wa Saikolojia ya Jamii, Dkt. Garvin Kweka alisema wazazi wengi kwa sasa wanalea watoto wasioweza kuhimili changamoto za maisha pamoja na hisia zao.
“Ndiyo maana siku hizi watoto wameanza kujiua. Hii ni kutokana na kutengeneza kizazi kisichoweza kuhimili maumivu kabisa. Nina takwimu kuwa mtoto wa kwanza mwenye umri mdogo kujiua alikuwa na miaka sita kutoka Mkoa wa Katavi,” alisema.
Aliongeza kuwa jamii inapaswa kuwajengea watoto uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha badala ya kuwalea katika mazingira yanayowafanya washindwe kuvumilia misukosuko mbalimbali ya maisha.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...