Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wafugaji nchini kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayotolewa katika kampasi zake pamoja na kuwafuata wafugaji moja kwa moja kwenye maeneo yao ili kuwajengea uwezo wa kufanya ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.

Akizungumza Mei 8, 2026, Jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa LITA, Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt. Pius Mwambene amesema taasisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kisasa kuwafikishia wafugaji elimu inayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mifugo nchini.

Amesema LITA ina mkakati wa kuwafuata wafugaji katika maeneo yao ili kubaini changamoto na mahitaji waliyonayo kwa wakati husika, huku mafunzo yanayotolewa yakizingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani.

“Tunatoa mafunzo yanayolenga kujibu mahitaji halisi ya wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo ili waweze kubadilisha mifumo yao ya ufugaji na kuingia kwenye ufugaji wa kibiashara zaidi”.

Aidha, amesema mifugo ni mali yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, hivyo amewahamasisha wafugaji kuendelea kutumia vyuo vya mifugo vilivyopo nchini kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu yatakayowawezesha kuongeza tija katika shughuli zao.

Katika mkutano huo, Dkt. Mwambene amesema mchango wa LITA katika sekta ya mifugo nchini ni mkubwa, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maafisa ugani wanaofanya kazi nchini wametokana na vyuo vya LITA na wamepata umahiri wao kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi hiyo.

Baraza la LITA linaundwa na kampasi nane ambazo ni Tengeru, Mpwapwa, Tanga, Mwanza, Songea-Madaba, Temeke, Morogoro na Kagera, awali taasisi hiyo ilikuwa ikidahili wanafunzi takribani 700 pekee, lakini sasa imefikia zaidi ya wanafunzi 3,000 nchini na Mgeni Rasmi katika Baraza hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi Agnes K. Meena.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...