Na Belinda Joseph -Dodoma.

Hafla ya kuhitimisha mafunzo ya mradi wa Rise Mamalishe imefanyika jijini Dodoma baada ya kuwafikia zaidi ya Mamalishe 3,000 kutoka mikoa mitano nchini, kupitia mradi uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu ukiratibiwa na Stanbic Bank.

Akizungumza Mei 19 Jijini Dodoma, katika hafla hiyo, Meneja wa Stanbic Bank tawi la Dodoma, Joan Mbise, amesema mradi huo umewawezesha Mamalishe kuendelea kufanya biashara zao kwa ufanisi huku wakiboresha maisha yao na kukuza uchumi wao.

Amesema kati ya Mamalishe hao, zaidi ya 2,000 wamefikiwa kupitia mikopo ya mzunguko, huku Mamalishe 200 tayari wakisajiliwa na SIDO, kupata vyeti pamoja na vitambulisho vinavyowatambua rasmi kama wajasiriamali.

“Lengo letu ni kuhakikisha ujuzi wao unaimarika, biashara zao zinakua na jamii inanufaika. Kupitia mafunzo haya wameweza kuongeza thamani ya biashara zao na kuendesha shughuli zao kwa weledi zaidi,” amesema Mbise.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mafunzo na usimamizi wa Mikoa, kutoka SIDO, CPA George Kasinga amesema programu ya Rise Mamalishe imekuwa chachu muhimu katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali na kukuza biashara ndogondogo nchini.

Amesema SIDO imeendelea kutoa mafunzo na ushauri kwa wafanyabiashara ili kuhakikisha wanapata ujuzi wa kuendeleza biashara zao pamoja na kuongeza ushindani sokoni.

Aidha, washiriki wa programu hiyo wamekuwa wakipatiwa elimu ya fedha, usalama wa chakula, mbinu za kuongeza thamani ya bidhaa na namna ya kuvutia wateja, hatua inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi na kuwasaidia kupata mikopo pamoja na matumizi sahihi ya mitaji.

Baadhi ya Mamalishe waliohitimu mafunzo hayo wameipongeza Stanbic Bank kwa kuandaa programu hiyo wakisema imewaongezea maarifa na ujuzi uliowasaidia kuongeza kipato na kuboresha huduma kwa wateja wao.

Wameahidi kutumia elimu waliyoipata kuwasaidia pia wafanyabiashara wengine katika jamii zao ili kuongeza maendeleo ya kiuchumi.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...