Na Farida Mangube

Kamishna wa Kamisheni ya Polisi Jamii, Alex Mkama, amesema mmomonyoko wa maadili katika jamii umeendelea kuwa moja ya vyanzo vinavyochochea uhalifu, rushwa na kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

Mkama amesema hayo katika Chuo cha Maafisa wa Polisi Kidatu (TPSC Kidatu), wilayani Kilombero mkoani Morogoro, wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi Mdogo Ngazi ya Sajini Awamu ya Pili ya mwaka wa mafunzo 2025/2026, ambapo askari 774 wamehitimu.

Amesema ili kulinda amani ya nchi, askari wa polisi wanapaswa kuwa waadilifu, waaminifu na wenye uwezo wa kusikiliza wananchi pamoja na kuwapatia mrejesho kuhusu hatua zinazochukuliwa katika mashauri yao.

Pia amewataka viongozi wa dini kuendelea kutumia majukwaa yao kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa maadili na ushiriki wa wananchi katika ulinzi na usalama wa nchi.

Mkama ameonya kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwa chanzo cha taharuki na kuhatarisha usalama wa taifa iwapo hayatadhibitiwa na kuwataka askari wasijiingize katika matumizi hayo mabaya.

Mkuu wa Chuo hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Zarau Mpangule, amesema mafunzo yaliyotolewa yamejikita katika mambo mbalimbali ikiwemo sheria, uchunguzi wa makosa ya jinai, haki za binadamu, polisi jamii, usalama barabarani, kupambana na ugaidi pamoja na mbinu za medani na kivita.

Amesema chuo kinaendelea kuimarisha uwezo wa wakufunzi wake, ambapo 17 wanaendelea na mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma ndani na nje ya nchi, ikiwemo Urusi, Korea Kusini, Uturuki na Singapore.

SACP Mpangule amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya askari, huku akiwataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kuongeza ufanisi katika kazi ya polisi na kuchangia maendeleo ya taifa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...