Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha kwa kiasi kikubwa maslahi ya watumishi wa umma na sekta binafsi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na tija kwa Taifa.

Akizungumza akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, Senyamule alibainisha kuwa maboresho hayo yanajumuisha ulipaji wa mishahara kwa wakati, upandishaji wa madaraja pamoja na ujenzi wa nyumba za watumishi.

Alieleza kuwa Serikali pia imeimarisha huduma za kijamii kwa watumishi, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara na mawasiliano, hasa kwa watumishi waliopo maeneo ya mijini na vijijini, ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Senyamule alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira bora na yenye motisha. Alitoa rai kwa waajiri wote, hususan wa sekta binafsi, kuzingatia sheria za ajira, ikiwa ni pamoja na kutoa mikataba rasmi na kulipa stahiki za wafanyakazi kwa wakati.

Aidha, aliwataka wadaiwa wa watumishi kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi.

“Maelekezo ya Rais ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuishi kwa tabasamu, na hilo linaanzia kwa watumishi wenyewe kuwa katika mazingira mazuri ya kazi,” alisema Senyamule.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Dodoma alisema Siku ya Wafanyakazi ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuwakumbusha waajiri wajibu wao kwa waajiriwa.

Akisoma risala ya wafanyakazi, Mratibu wa TUCTA Dodoma, Audax Stephano Stanslaus, aliishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha maslahi ya watumishi, ikiwemo kupandisha madaraja na kutoa ruzuku.

Hata hivyo, alibainisha kuwepo kwa changamoto kadhaa, zikiwemo ucheleweshaji wa malipo ya likizo, fedha za kujikimu kwa watumishi wapya, pamoja na stahiki za watumishi wanaorejea kazini baada ya masomo.

Alisema wafanyakazi wana matumaini kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto hizo na kuboresha zaidi mishahara ili kuinua hali zao za maisha.

Sherehe hizo kwa mkoa wa Dodoma, zilianza kwa maandamano kutoka viwanja vya Bunge hadi Uwanja wa Jamhuri, zikihusisha wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali mkoani Dodoma.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...