Na Janeth Raphael- MichuziTv
Rais wa Kenya, William Ruto, ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kuunda tume maalum ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi, Rais Ruto alisema uamuzi huo unaakisi uongozi thabiti, wenye uwajibikaji na unaozingatia misingi ya kisheria katika kushughulikia changamoto za kitaifa. Alieleza kuwa kuundwa kwa tume hiyo ni ishara ya dhamira ya dhati ya serikali ya Tanzania katika kuhakikisha ukweli wa matukio unajulikana na haki inatendeka kwa wote.
Tume hiyo, inayojulikana kama Tume ya Jaji Othman Chande, inalenga kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vurugu na matukio mengine yaliyoathiri utulivu wa nchi katika kipindi hicho nyeti cha uchaguzi. Rais Ruto alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga msingi imara wa amani, uwajibikaji na maridhiano ya kitaifa.
Aidha, kiongozi huyo wa Kenya alibainisha kuwa juhudi hizo zinaungwa mkono na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kulinda amani, kuimarisha ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa ukanda huo.
Akirejea uzoefu wa Kenya katika vipindi vya changamoto za kisiasa, Rais Ruto alieleza imani yake kuwa Tanzania itaweza kuvuka hali hiyo na kuibuka imara zaidi. Pia aliahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya Kenya na Tanzania katika kuimarisha utawala bora, amani na maendeleo endelevu.
Kuundwa kwa tume hiyo ni sehemu ya juhudi pana za Serikali ya Tanzania kuhakikisha matukio yote yaliyojitokeza yanachunguzwa kwa uwazi na haki, huku ikiweka msingi wa kudumu wa utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...