Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma

Serikali imesema itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa sera, sheria na miongozo inayohusu huduma za lishe nchini, ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi na salama kuhusu afya na lishe.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la papo kwa hapo lililoulizwa na Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe kuhusu ongezeko la watu wanaojihusisha na utoaji wa huduma za lishe bila kuwa na vibali au sifa stahiki.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na mabaraza na taasisi za kitaalamu itaendelea kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazohusu huduma za afya na lishe zinafuatwa kikamilifu ili kuwalinda wananchi dhidi ya taarifa potofu au huduma zisizo salama.

“Niwaelekeze Wizara ya Afya pamoja na mabaraza yote ya kitaalamu kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, sera na miongozo ya huduma za lishe huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini kuhusu uwezekano wa kuratibu vizuri zaidi masuala ya leseni kwa watoa huduma za afya na lishe,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojitangaza kuwa wataalamu wa lishe kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kukua kwa utandawazi pamoja na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, pamoja na faida zinazotokana na upatikanaji wa taarifa kwa urahisi kupitia teknolojia, bado ipo haja ya kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu lishe inatolewa na wataalamu wenye sifa, weledi na vibali vinavyotambulika kisheria.

Aidha, amesema Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watu au taasisi zitakazobainika kutoa huduma za lishe kinyume na taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa wataalamu waliosajiliwa na mamlaka husika.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa afya za wananchi pamoja na kuhakikisha elimu ya lishe inayotolewa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...