Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma
Serikali imesema inaendelea kuimarisha mfumo wa usuluhishi wa migogoro ya ndoa nchini ili kupunguza ucheleweshaji wa mashauri ya talaka na kusaidia wanandoa kupata suluhu kabla ya kufikishana mahakamani.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amesema hayo leo Mei 7, 2026 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Happiness Ngwando, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ili kuharakisha umalizaji wa kesi za talaka.
Mhe. Katimba amesema kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa, Sura ya 29, kinaitafsiri ndoa kuwa ni muunganiko wa mwanamke na mwanaume kwa lengo la kuishi pamoja maisha yote, hivyo sheria hiyo imeweka utaratibu wa mashauri ya ndoa kuanza kusikilizwa katika Bodi za Usuluhishi wa Ndoa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Amesema lengo la utaratibu huo ni kutoa nafasi ya maridhiano na kutafuta suluhu badala ya wanandoa kuachana haraka.
Aidha, amesema Mahakama ya Tanzania imeweka mwongozo maalumu wa muda wa usikilizaji wa kesi ili kuharakisha utoaji wa haki. Kwa mujibu wa mwongozo huo, mashauri katika Mahakama za Mwanzo yanapaswa kukamilika ndani ya miezi sita, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi ndani ya mwaka mmoja, huku Mahakama Kuu ikiwa na ukomo wa miaka miwili.
“Mashauri ya talaka pia yanaweza kusikilizwa na kuamuliwa katika Mahakama za Mwanzo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” amesema Mhe. Katimba.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeanza programu ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa nchi nzima ili kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya kifamilia.
Amesema utekelezaji wa programu hiyo ulianza rasmi Aprili 8, 2026 mkoani Kagera, ukiwa na lengo la kuhakikisha wanandoa wenye migogoro wanapata ushauri na suluhu stahiki kabla ya kufungua mashauri ya talaka mahakamani.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...