Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni- Dodoma.

Serikali imesema kuwa Makao yote ya Watoto nchini yanaanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo maalum inayolenga kuhakikisha watoto wanaolelewa katika vituo hivyo wanaishi katika mazingira salama, yenye ulinzi na malezi bora.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 25, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Winfried Mahundi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Simirya Kombani ambaye alitaka kujua ni utaratibu gani unaotumiwa na Serikali kuhakikisha watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto wanapata mazingira bora na salama.

Akijibu swali hilo, Mahundi amesema Makao yote ya Watoto yanaanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Kanuni za Makao ya Watoto za mwaka 2012 pamoja na Mwongozo wa Taifa wa Uanzishaji, Uendeshaji na Usimamizi wa Makao ya Watoto wa mwaka 2024.

Amesema utaratibu wa kuanzisha Makao ya Watoto huanzia ngazi ya Kata ambapo maombi hupokelewa na kufanyiwa tathmini kabla ya kuwasilishwa katika ngazi ya Halmashauri na hatimaye kupelekwa Wizarani kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupata leseni ya usajili.

“Makao hayo hupatiwa usajili rasmi pale yanapokidhi vigezo na masharti yote yaliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki za malezi, ulinzi na maendeleo yao kwa ujumla,” amesema Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa Makao ya Watoto kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii waliopo katika ngazi mbalimbali kuanzia Wizara, Mkoa hadi Halmashauri.

Kwa mujibu wa Mahundi, Maafisa hao hufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika vituo vya kulelea watoto ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vya ubora pamoja na kulinda haki na usalama wa watoto wanaolelewa humo.

Amesisitiza kuwa Serikali haitaruhusu uwepo wa Makao ya Watoto yanayokiuka taratibu, sheria na miongozo iliyowekwa kwani lengo kuu ni kuhakikisha watoto wote wanaopata huduma katika vituo hivyo wanalelewa katika mazingira yenye upendo, usalama na ustawi unaostahili.

Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya malezi na ulinzi wa watoto nchini, sambamba na kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na huduma za watoto zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na misingi ya haki za mtoto.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...