Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
OFISA Uchunguzi wa Halotel Fabian Kulwa (40) na wenzane watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwemo kutumia namba za NIDA za wateja kusajilia laini za watu wengine na kutakatisha fedha Sh milioni 355.
Mbali na Kulwa anayeishi Mbezi Makabe washtakiwa wengine ni Gilbert Nyamitah (33) Mkazi wa Madale, Mnyamisi Selumamala (34), Mkazi wa Musoma Mara, Salum Kapene (31) Ofisa Masoko wa Halotel Mkazi wa Mwanza, Onesmo Aron (34) mfanyakazi huduma huru Mkazi wa Runzewe Geita na Joram Fanuel (23) Mkazi wa Tarime Mara.
Watuhumiwa hao wakiongozwa na mshtakiwa wa kwanza Nyamitah ambae ni mlemavu wa miguu anayetumia kiti cha magurudumu wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Michael Shindai amedai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei, Julai, 2025 na Aprili 2026 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amedaiwa washtakiwa wanatuhumiwa kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu, kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, kutumia vibaya taarifa za mteja na kutakatisha fedha.
Imedaiawa katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wote, kati ya Mei Mosi, 2025 katika mahali pasipojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makusudi
waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia taarifa za wateja na laini za simu zilizokuwa na usajili wa watu wengine.
Katika shtaka la pili hadi la 18 mshtakiwa Nyamitah anaiwa, Machi 31,2026 alitumia laini zilizosajiliwa kwa jina la mtu mwingine akiwa Madale ndani ya Wilaya Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam bila ya kumjulisha mtoa huduma.
Imedaiwa kuwa alitumia laini iliyosajiliwa kwa jina la Kwimba Maduhu, Bhoke Ryoba, Daniel Ng'era, Chacha Mbango, Zainabu Burunya, Manga Marwa, Bhoke Mwita, Verynice Nyaonge, Masele Kinga, Charles Genga na Latifa Athumani.
Wakili Shindai aliendelea kudai kuwa katika shtaka la 19 hadi 27 mshtakiwa Majige, akiwa mfanyakazi huru wa Kampuni ya Honora Tanzania PLC alitumia namba ya NIDA ya Tagambi Bungulwa kusajili namba 0714-643547 kosa analodaiwa kulitenda Mei Mosi, 2025 huko Wilaya Busega mkoani Simiyu
Pia, anatuhumiwa kutumia namba za watu wengine za NIDA za Joseph Mwita, Bhoke Mwita, Manga Marwa, Kwimba Maduhu, Bhoke Roba, Daniel Ng'era, Chacha Mbango na Zainabu Burunya.
Katikati shtaka la utakatishaji fedha, Nyamitah na Kulwa wanadaiwa wakiwa mahali pasipojulikan ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja walifanikiwa kupata Sh milioni 355 huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la uhalifu wa kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi bado haujamilika.
"Mshtakiwa wa kwanza (Nyamitah) na wa pili (Kulwa) nyie hamna dhamana kwa sababu mna shtaka la utakatishaji fedha, mliyobaki kila mmoja anatakiwa awe na wadhami wawili kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni tano,"amesema Hakimu Nyaki
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.





.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...