Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya kufuatia kusainiwa kwa mikataba minane yenye lengo la kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 4, 2026 baada ya mazungumzo ya kitaifa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, Rais Samia alisema nchi hizo mbili zimekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyokwamisha biashara ya mipakani na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Alieleza kuwa mazungumzo yao yalijikita zaidi katika ajenda za kiuchumi zinazogusa moja kwa moja ustawi wa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa Kamati za Pamoja za Biashara kuendelea kukutana mara kwa mara ili kutatua changamoto na kuzuia kuibuka kwa vikwazo vipya.
Katika hatua muhimu ya ushirikiano huo, mikataba iliyosainiwa inahusu sekta za nishati, miundombinu na uchukuzi, ulinzi pamoja na TEHAMA. Rais Samia alibainisha kuwa katika sekta ya nishati, nchi hizo zimekubaliana kuendeleza miradi ya kuunganisha umeme, ambapo njia moja tayari imekamilika na maandalizi ya mradi wa pili yanaendelea.
Kwa upande wa miundombinu, makubaliano yamefikiwa ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, pamoja na kuunganisha reli kutoka Bandari ya Tanga kupitia Kilimanjaro hadi Kenya. Aidha, Kenya itaunganisha mtandao wake wa reli na kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) cha Tanzania kutoka Singida, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria.
Katika sekta ya usafiri wa majini, Tanzania na Kenya zimekubaliana pia kuimarisha usafiri katika Ziwa Victoria ili kurahisisha biashara kati ya nchi hizo pamoja na Uganda, jambo litakaloongeza ushindani wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ziara ya Rais Ruto nchini Tanzania imeelezwa kuwa ni ishara ya dhamira ya dhati ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, huku ikifungua ukurasa mpya wa fursa za maendeleo kwa wananchi wake.
Hatua hii inaonekana kuwa kichocheo muhimu cha kukuza uchumi wa kikanda na kuimarisha ushirikiano wa Afrika Mashariki katika sekta mbalimbali za maendeleo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...