Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema ameridhishwa na mafanikio ya Shindano la Ubunifu lililoanzishwa na Wizara yake kwa lengo la kuwashirikisha wanafunzi wa fani za uhandisi na ujenzi katika kutoa mawazo ya maendeleo ya miundombinu nchini.
Akizungumza kuhusu dhamira ya shindano hilo, Ulega amesema lengo kuu lilikuwa ni kukutana na wanafunzi wa taaluma za uhandisi pamoja na ukadiriaji majengo ili kuwapa uelewa kuhusu miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali, sambamba na kusikiliza maoni na ubunifu wao kuhusu maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Ulega Amezungumza hayo jijini Dodoma wakati wa hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa Shindano la andiko la ubunifu wa kupunguza msongamano wa magari mijini ambapo amesema wakati wa kuanzisha mpango huo kulikuwa na baadhi ya watu waliobeza hatua hiyo wakidai Serikali haina mipango madhubuti hadi kufikia hatua ya kutafuta mawazo kutoka kwa wanafunzi, huku baadhi ya viongozi wa upinzani wakikosoa vikali mpango huo.
Hata hivyo, Ulega amesema Wizara imeamua kuwapa nafasi vijana kutokana na uwezo wao mkubwa wa kufikiri, kubuni na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazohusu maendeleo ya Taifa.
Amesema mwitikio wa wananchi na wadau ulikuwa mkubwa, hali iliyosababisha Wizara kupokea simu nyingi za pongezi kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali zilizovutiwa na hatua ya kuwashirikisha vijana katika masuala ya maendeleo ya miundombinu.
Aidha, amesema mafanikio ya shindano hilo yamevutia taasisi mbalimbali ikiwemo mabenki kuamua kuunga mkono mpango huo kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi na washiriki, zikiwemo fedha taslimu za mamilioni ya shilingi pamoja na kompyuta mpakato.
Ulega amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhimiza ubunifu na ushiriki wa vijana katika ujenzi wa Taifa, jambo lililoipa Wizara motisha ya kuendelea kutoa nafasi kwa vijana kushiriki katika miradi ya maendeleo.
Pia amesema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda alimpongeza kwa hatua hiyo kupitia simu na hata kumwandikia barua rasmi ya pongezi, jambo alilosema lilimpa faraja kubwa.
Kwa mujibu wa Ulega, Profesa Mkenda alieleza kuwa lengo la challenge hiyo ni kuhamasisha matumizi ya maarifa ya vijana, kuwasaidia wanafunzi kuunganisha nadharia wanazojifunza darasani na vitendo pamoja na kuchochea ubunifu katika sekta ya miundombinu.
Amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha vijana kila inapopata nafasi kwa kuwa Tanzania ina wataalamu wengi wenye uwezo mkubwa katika sekta ya ujenzi na miundombinu.
“Wizara ya Ujenzi ni walezi wa wahandisi wote nchini. Tuna taarifa zenu zote na tutaendelea kuwalea kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu,” amesema Ulega.
Katika hatua nyingine, amesema Wizara ipo katika mazungumzo na wadau wa kimataifa kwa ajili ya kuandaa “master plan” ya kisasa ya madaraja na barabara yenye lengo la kujenga miundombinu ya kiwango cha kimataifa.
Ameeleza kuwa mwelekeo wa Serikali sasa ni kutoka mfumo wa barabara moja kwenda mfumo wa barabara pana zaidi zenye njia mbili kwenda na mbili kurudi ili kukidhi mahitaji ya ukuaji wa miji pamoja na uchumi.
“Kina nani wa kufanya kazi hiyo? Ni wataalamu hawa tulionao leo pamoja na ninyi mliopo madarasani,” amesema.
Aidha, amesema Serikali ya Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwaamini vijana kwa kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi, akibainisha kuwa karibu nusu ya mawaziri waliopo serikalini ni vijana wenye umri wa miaka 50 na chini yake.
Ulega amesema kupitia shindano hilo, vijana wengi watafunguliwa milango ya ajira na kujiajiri kupitia ubunifu na ushiriki wao katika miradi mikubwa ya maendeleo nchini.



.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...