Na Janeth Raphael MichuziTv- Bungeni Dodoma

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, ameainisha vipaumbele nane vitakavyoongoza utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Ulinzi katika mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuimarisha uwezo wa kiulinzi, kuendeleza Jeshi, pamoja na kuhakikisha usalama wa Taifa unaimarishwa kwa kiwango cha juu zaidi.

Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, Dkt. Nyansaho amesema Serikali imeweka mkazo katika kuboresha na kuimarisha Jeshi la Ulinzi kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa vya kijeshi, teknolojia ya kisasa ya mawasiliano pamoja na kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha Jeshi linakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama za sasa na zijazo, ambazo zinabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya kikanda na kimataifa.

Katika upande wa ustawi wa wanajeshi, Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi kupitia matunzo bora ya vifaa na zana za kijeshi, mafunzo ya mara kwa mara, pamoja na mazoezi ya kijeshi yenye kuendana na viwango vya kimataifa.

Aidha, amebainisha kuwa huduma za afya, makazi na maslahi ya wanajeshi kwa ujumla pia yataendelea kupewa kipaumbele ili kuongeza morali, nidhamu na ufanisi katika utendaji kazi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kuhusu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Nyansaho amesema Serikali imejipanga kuongeza uwezo wa jeshi hilo kwa kuboresha miundombinu yake ili kuwezesha vijana wengi zaidi kupata fursa ya mafunzo ya awali ya kijeshi sambamba na stadi mbalimbali za kazi zitakazowawezesha kujitegemea baada ya mafunzo.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii na kiulinzi, huku JKT likiendelea kuwa chombo muhimu katika malezi ya uzalendo na nidhamu kwa vijana wa Kitanzania.

Katika kuimarisha ulinzi wa Taifa, Waziri Nyansaho pia amesema Jeshi la Akiba litaendelea kuimarishwa ili kuongeza utayari wake wa kushiriki katika ulinzi wa nchi pale litakapohitajika, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa kiulinzi wa ndani.

Aidha, Wizara hiyo itaendelea kulinda na kuendeleza miradi ya kimkakati ya Taifa ili kuhakikisha inatoa mchango chanya katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi.

Pamoja na hayo, Serikali itaendelea kuboresha taasisi na mashirika yanayojihusisha na utafiti wa masuala ya kijeshi, sambamba na kuanzisha viwanda vipya vya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa za kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Kwa mujibu wa Dkt. Nyansaho, hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa bidhaa za ulinzi kutoka nje ya nchi na kuimarisha uwezo wa ndani wa uzalishaji wa teknolojia na vifaa vya kiulinzi.

Kuhusu ushirikiano wa kimataifa, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na mataifa mbalimbali duniani katika masuala ya ulinzi na usalama.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiusalama za kikanda na kimataifa, ikiwemo ugaidi, uhalifu wa kimataifa na majanga ya kibinadamu.

Aidha, Wizara ya Ulinzi itaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali pale yanapotokea, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usalama na ustawi wa wananchi.

Kwa ujumla, vipaumbele vilivyoainishwa na Wizara hiyo vinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha Jeshi la Ulinzi, kukuza uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mazingira salama na imara kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...