-Agusia korosho za Tanzania zinavyopendwa nchini Urusi ,raia wa nchi hiyo walivyoonesha upendo wao kwa Rais 

-Mchambuzi wa siasa za kimataifa naye aweka wazi muonekano wa Tanzania kupitia ziara ya kihistoria

Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

KAMA kuna jambo limeleta faraja na kuleta matumaini katika mioyo ya Watanzania basi ni hii ziara ya kihistoria iliyofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan .

Ni ziara ambayo kwa hakika imeenda kufungua milango na fursa kwa Taifa la Tanzania na Rais Dk.Samia akiwa nchini Urusi ametoa hotuba iliyobeba maono na dhamira yake njema kwa Taifa lake na kwa kubwa zaidi kwa kuangalia maslahi mapana kwa nchi zote mbili ,Tanzania na Urusi.

Binafsi kama ilivyo kwa Watanzania wengine wengi,nimekuwa nikifuatilia kwa karibu ziara ya Rais Samia nchini Urusi pamoja na kusikiliza kwa makini yaliyozungumzwa katika ziara hiyo .Kwa mujibu wa ratiba Rais Samia anarejea nchini leo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye ni miongoni mwa waandishi wa habari walioambatana na Rais Samia katika ziara hiyo ametumia nafasi yake kueleza kwa kina faida ya ziara ya Rais na hakika amezungumza hatua kwa hatua kuhusu aliyoyaona katika ziara hiyo.

Balile amesema ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefungua milango mipya ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani.

Anasema tayari bidhaa za Tanzania, hususan korosho, zimeanza kupata soko kubwa nchini Urusi huku wafanyabiashara wa nchi hiyo wakionyesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani mazao hayo.

“Nipo hapa katika maduka makubwa ya biashara na nimejionea korosho kutoka Tanzania zikipewa kipaumbele.Wafanyabiashara wengi wameonyesha nia ya kuja kuwekeza katika viwanda vya kubangua na kufungasha korosho ili ziweze kuuzwa kwa ubora zaidi katika soko la Urusi,” anasema Balile.

Anaongeza mbali na korosho, wawekezaji wa Urusi wameonyesha hamu ya kuwekeza katika sekta za chai, kahawa na kilimo kwa ujumla, jambo ambalo linaweza kuwanufaisha wakulima wa kawaida na kuongeza uhakika wa masoko ya mazao ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Balile, ziara hiyo ni ya kihistoria kwani imefanyika takribani miaka 57 baada ya ziara ya mwisho ya kiongozi wa Tanzania nchini ambayo iliyofanywa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Balile anasema mapokezi ya Rais Samia na ujumbe wake nchini Urusi yanaonyesha namna ambavyo wananchi wa Urusi wanavyothamini uhusiano wao na Tanzania.

“Wananchi wa kawaida wameguswa sana na ujio wa Rais Samia. Wengi wanatueleza kuwa ujio huu umeonyesha kuwa bado wana marafiki wa kweli duniani. Vyombo vya habari vya Urusi vimeipa Tanzania nafasi kubwa na watu wengi wanahoji kuhusu uhusiano wetu na Urusi,” anasema Balile ambaye alieleza hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha U FM cha Azam Media.

Balile pia anaeleza kwamba mpango wa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Urusi unaweza kuongeza idadi ya watalii na kuchochea biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Akitoa tathmini yake kuhusu ziara hiyo, mchambuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia, Godfrey Mchungu, anasema l ziara ya Rais Dk.Samia ni ya kimkakati na inaendana na mwelekeo wa Tanzania wa kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Anasema Urusi ni moja ya mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani katika sekta za nishati, teknolojia, biashara na siasa za kimataifa, hivyo ushirikiano wake na Tanzania unaweza kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi.

“Hii ni ziara inayojenga msingi wa kuimarisha sera ya nje ya Tanzania kwa kuzingatia diplomasia ya uchumi. Tanzania inahitaji kushirikiana na mataifa yenye nguvu za kiuchumi na kiteknolojia ili kuongeza uwekezaji, biashara na maendeleo ya sekta mbalimbali.”

Anaongeza ushiriki wa Rais Dk.Samia katika majukwaa makubwa ya kimataifa nchini Urusi umeongeza mwonekano wa Tanzania duniani na kutoa fursa ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyopo nchini.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, mafanikio ya ziara hiyo yatategemea namna ambavyo makubaliano yaliyofikiwa yatatekelezwa kwa vitendo kupitia ushirikiano wa wataalamu wa pande zote mbili.

“Ziara na mazungumzo ni hatua ya kwanza. Hatua inayofuata ni kwa wataalamu kuchakata makubaliano hayo na kuyaweka katika utekelezaji. Hapo ndipo Watanzania wataanza kuona matokeo halisi ya ushirikiano huo katika sekta za elimu, afya, teknolojia, nishati, biashara na uwekezaji,” anasema.

Ziara ya Rais Samia nchini Urusi imehusisha mikutano ya ngazi ya juu, mazungumzo ya kibiashara na uwekezaji pamoja na ushiriki katika majukwaa ya kimataifa, huku ikilenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Urusi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi.

Simu 0713833822










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...