-Uwekezaji wa Bil 49/- NIRC unavyookoa wakulima wadogo Korogwe
Na Hafidh Kido
MOSES Mdoe amesimama mbele ya mfereji unaotiririsha maji kwa kasi, sauti yake inatengeneza mwagwi unaotufanya tuzungumze kwa sauti za juu wakati wa mahojiano.
“Hii ni baraka aliyotujaalia Mungu wananchi wa Kijiji hiki. Dunia ipo kwenye mtanziko wa athari za mabadiliko ya tabianchi lakini sisi baraka ndio kama hii, maji yanatiririka tunapata mavuno,” anasema Mdoe.
Nyuma ya maneno ya faraja ya Mdoe ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekelei, Kata ya Chekelei, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, kuna kilio cha muda mrefu kwa wakulima wa mpunga, mbogamboga na matunda juu ya skimu kongwe ya umwagiliaji.
“Skimu ya kwanza ya jadi na miundombinu ya kienyeji ya umwagiliaji hapa Chekelei ilianza kujengwa na kutumiwa na wakulima wenyewe tangu mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka 1980, ambapo wakulima walitegemea mifereji ya udongo iliyochimbwa kwa mkono kuelekeza maji kutoka milimani,” anaeleza Mdoe.
Kwa mujibu wa taarifa za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), baada ya serikali kuona juhudi za wananchi skimu hiyo ilianza kufanyiwa maboresho rasmi ya kitaalamu kati ya mwaka 1996 na 1997, ambapo serikali kwa ushirikiano na wafadhili ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Mradi wa Ushirikishwaji, Maendeleo na Uwezeshaji katika Sekta ya Kilimo (PADEP) ilijenga baadhi ya mifereji ya zege ili kupunguza upotevu wa maji ardhini.
Aidha, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Kata ya Chekelei ina jumla ya wakazi wapatao 9,778.
Kwa miaka mingi Chekelei inafahamika ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kama moja ya ghala la chakula au kitovu kikubwa cha uzalishaji wa nafaka, hasa mpunga.
Pamoja na mpunga, wakulima wa Chekelei wanalima mazao ya chakula kama mahindi, na mazao ya bustani ya muda mfupi kama vile matango, pilipili hoho na matikiti maji hasa kwenye maeneo yenye mwinuko kidogo kipindi cha kiangazi.
Jiografia ya Chekelei inafanya kijiji hiki kupokea maji mengi yanayotiririka kutoka safu za Milima ya Usambara.
Wakati wa mvua kubwa, maji yanakuwa mengi mabondeni, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni kukosekana kwa miundombinu thabiti ya kuyazuia na kuyahifadhi, hivyo maji yalipita kwa wingi na kuleta athari kama mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na kuondoa udongo wenye rutuba.
Mvua zinapokata au kuchelewa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, wakulima hukumbana na ukame.Hali hii hulazimisha mbegu kukauka ardhini na kusababisha hasara, hivyo kuwafanya wakulima wajitegemee kwa miundombinu ya kienyeji au kubadili mazao kama kulima matikiti yanayostahimili maji kidogo.
Mwanaisha Zuberi mkazi wa Chekelei, ni mkulima wa mpunga na mahindi kwa miaka tisa sasa, anasimulia adha wanayopata kutokana na kuyumba kwa misimu ya mvua.
"Kuna miaka mvua zinakuwa nyingi sana na siku nyingine zinakuwa chache hadi hatupati chakula; kwa ufupi mvua hazina msimamo," anasema Mwanaisha.
Anaongeza kuwa kwa sasa wanategemea sana taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia redio, ambapo viongozi wa kijiji wanapozipata huwashauri kupanda mazao yanayohimili mabadiliko hayo.
Changamoto ya ukame wa ghafla inathibitishwa pia na Goodluck Kaoneka, mkulima wa mazao ya mboga mboga na matunda ikiwemo matango, pilipili hoho na matikiti katika kata hiyo.
Kaoneka anaeleza mvua zikikata, mbegu hushindwa kuota na kuwasababishia hasara kubwa, hatua inayowalazimu kusitisha kilimo.
"Maji yanapokata inabidi ulime katika kipindi ambacho mbegu zinaweza kutoka kwa haraka. Ndio maana tikiti halichukui maji mengi, hivyo tunalilima zaidi kipindi cha mvua chache," anabainisha Kaoneka akieleza mbinu mbadala wanazotumia sasa kujinusuru walizoelezwa na wataalamu wakilimo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chekelei, Mdoe anafafanua kuwa tatizo kubwa halijawahi kuwa ukosefu wa maji kabisa, bali ni ukosefu wa miundombinu ya kuyahifadhi. Wakati wa masika, maji yanakuwa mengi lakini yanapita na kuondoka kwa kasi kwa kuwa hakuna kizuizi.
"Baadhi ya miundombinu wakulima wanajitengenezea wenyewe kienyeji. Wakulima wanakuwa mabondeni na wengine wako juu, jambo linaloleta usumbufu," anasema Mdoe.
Ushirikiano kati ya wakulima na wataalamu wa kilimo umekuwa nguzo muhimu.
Mdoe anamsifia Afisa Kilimo wa eneo hilo, Juma Mashauri, akisema: "Anajitahidi sana. Hata masuala ya mbolea yanatumwa kwa njia ya ujumbe wa maandishi (SMS) kwenye simu, na anatupa muongozo kukiwa na changamoto ya wadudu au mvua kuchelewa."
NIRC inaibuka kama mkombozi
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia usalama wa chakula na ustawi wa kiuchumi nchini, Serikali ya Awamu ya Sita imeelekeza uwekezaji mkubwa wa kimkakati wa zaidi ya Shilingi bilioni 49.7 katika miradi ya miundombinu ya umwagiliaji wilayani Korogwe.
Hatua hii inalenga kuwatoa wakulima wadogo katika utegemezi wa kilimo cha mvua za msimu na kuwaingiza katika kilimo endelevu chenye tija ya kibiashara.
Kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), miradi miwili mikuu ya Bwawa la Mkomazi na ukarabati wa skimu ya Chekelei inatajwa kuwa mkombozi wa mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula na biashara kwa maelfu ya kaya vijiduniani.
“Mradi huu unaolenga kujibu kilio cha wakulima wa mpunga waliopo mabondeni na vilimani. Serikali imetenga kiasi kikubwa cha fedha ili kuleta suluhisho la kudumu la uhifadhi wa maji,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mdolwa.
Anafafanua kuwa mradi wa Chekelei utagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 31.1, ambapo tayari umeshaanza kutekelezwa na umefikia asilimia 10.01.
“Mradi huu utanufaisha wananchi 4,000 katika vijiji sita vya Kata ya Chekelei. Mradi unatarajiw akuikamilika Machi 2027,” anasema Mdolwa.
Mwenyekiti Mdoe anabainisha ujenzi wa bwawa hili unaleta matumaini makubwa: "Ukikamilika huu mradi wa bwawa tutakuwa na maisha mazuri, tutalima kwa wakati na tutavuna kwa wakati."
NIRC hawajaishia hapo katika Wilaya ya Korogwe, mradi mwingine unatekelezwa Mkomazi, ambapo kwa mujibu wa NIRC mradi huu unalenga ukanda mpana zaidi wa wilaya hiyo na upo ukingoni mwa kuanza kutoa matokeo.
Gharama zake ni Shilingi Bilioni 18.6, utekelezaji wake umefikia asilimia 97 wanufaika ni wananchi 20,000 katika vijiji 28 vilivyopo katika kata saba za Wilaya ya Korogwe na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu (2026).
Kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu kutoka NIRC, miradi hii inakwenda kuwasaidia wakulima wadogo kujipatia kipato cha uhakika zaidi kupitia kilimo cha mismu mitatu.
“Miundombinu hii itawawezesha wakulima kulima na kuvuna zaidi ya mara moja kwa mwaka, bila kusubiri wala kutegemea msimu wa mvua,” anasema Mdolwa.
Kuhama kutoka kilimo cha kienyeji cha mabondeni kwenda kwenye skimu rasmi zilizopangwa kunasaidia pia kulinda mazingira. Kunazuia uharibifu wa vyanzo vya maji na mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mafuriko ya msimu, huku kukihakikisha ugawaji wa maji wa usawa kati ya wakulima wa juu na wale wa chini wa skimu.
Ujenzi na ukarabati huu wa skimu za umwagiliaji wilayani Korogwe ni kielelezo tosha kuwa uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi unawezekana pale tu takwimu, rasilimali fedha, na ushiriki wa jamii vinapokutana pamoja.


Mwandishi wa makala haya (kulia) akiwa na mkulima wa mbogamboga na matunda, Goodluck Kaoneka. Ambaye anadai Kijiji cha Chekelei kitanufaika kiuchumi baada ya kukamilika mradi wa skimu ya umwagiliaji unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...