Na Janeth Raphael MichuziTv .
Serikali imezindua rasmi programu ya Grand Challenges Tanzania, jukwaa jipya la kitaifa litakalolenga kuimarisha utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kwa lengo la kupata suluhu endelevu za changamoto zinazoikabili jamii katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema mpango huo unafungua fursa mpya kwa watafiti, wabunifu na taasisi za Kitanzania kuibua na kuendeleza teknolojia pamoja na tafiti zenye matokeo yatakayoboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Aidha, amesema uzinduzi wa programu hiyo unaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotambua nafasi ya sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu kama nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Pia aliipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), The Science for Africa Foundation, Taasisi ya Afya ya Ifakara pamoja na washirika wengine wa maendeleo kwa kushirikiana kuanzisha mpango huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema kila kizazi hukabiliwa na changamoto zake, huku kizazi cha sasa kikikabiliwa na masuala ya usalama wa chakula, afya, ajira kwa vijana, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya fursa zinazotokana na mapinduzi ya kidijitali. Alisisitiza kuwa wataalamu, taasisi za utafiti na wabunifu wa Tanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kubuni suluhisho zinazolingana na mazingira na mahitaji ya nchi.
Dkt. Nungu amesema Grand Challenges Tanzania inalenga kuwakutanisha watafiti, wabunifu, watunga sera, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na jamii kwa ujumla ili kushirikiana kutafuta majibu ya changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja. Kwa mujibu wake, mafanikio ya jukwaa hilo yatategemea uwezo wa kubadilisha maarifa yanayotokana na tafiti na ubunifu kuwa matokeo yenye manufaa kwa wananchi.
Amebainisha kuwa Tanzania tayari imeweka msingi imara katika sekta ya sayansi na teknolojia kupitia uwekezaji uliofanyika kwa miaka kadhaa. Zaidi ya shilingi bilioni 129 zimehamasishwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kusaidia tafiti, maendeleo ya teknolojia, ubunifu na miundombinu ya kisayansi, huku Serikali ikichangia zaidi ya shilingi bilioni 85. Uwekezaji huo umewezesha kuanzishwa kwa maabara, vituo vya ubunifu na programu za kuwajengea uwezo watafiti pamoja na vijana wabunifu.
Sambamba na uzinduzi huo, COSTECH imetangaza kuwa itazindua Wito wa Kwanza wa Utafiti wa Grand Challenges Tanzania utakaowapa nafasi watafiti na wabunifu kuwasilisha mawazo bunifu yenye uwezo wa kutoa suluhisho kwa changamoto halisi za maendeleo. Kipaumbele kitawekwa kwa miradi inayohusisha ushirikiano wa taaluma mbalimbali pamoja na ushiriki wa vijana watafiti, wabunifu chipukizi, wanawake wanasayansi na taasisi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Serikali imeeleza kuwa mafanikio ya Grand Challenges Tanzania yatapimwa kwa kiwango ambacho tafiti na ubunifu vitachangia kuboresha afya, ustawi wa jamii, usalama wa chakula, uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi, huku ikitoa wito kwa wadau wa sekta za umma na binafsi kuendelea kushirikiana kuendeleza ajenda ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.





.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...