Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara kuwa makini wanapowapokea wageni katika maeneo yao ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuwapokea watu wasiowafahamu vizuri.

Kihongosi ametoa wito huo leo Juni 2,2026 aliposhiriki kikao cha Shina namba Mbili Kata ya Bonga wilayani Babati mkoani Manyara.

Akizungumza mara baada ya kusikiliza ajenda ya kikao hicho Kihongosi amesema pamoja na kwamba Watanzania wana sifa ya ukarimu na upendo kwa wageni, ni muhimu kuhakikisha wageni wanaopokelewa wanajulikana na hawana nia ya kuleta matatizo katika jamii.

“Nimeelezwa kwamba mnawapokea wageni wanaofika katika maeneo yenu na kuwachukulia kama ndugu. Hilo ni jambo jema na linaonyesha ukarimu na mshikamano uliopo katika jamii yetu,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa ukarimu huo unapaswa kuambatana na tahadhari ili kulinda usalama wa wananchi na maeneo yao.

“Hata hivyo, mnapopokea wageni ni muhimu kuchukua tahadhari na kujiridhisha kuwa ni watu salama. Tusije tukawapokea watu wenye nia mbaya au wahalifu ambao wanaweza kuleta matatizo katika maeneo yetu,” amesema.

Kihongosi amesisitiza kuwa viongozi wa maeneo na wananchi wanapaswa kushirikiana kuhakikisha taarifa za wageni wanaoingia katika jamii zinajulikana ili kuimarisha ulinzi na usalama.

“Ni wajibu wa viongozi na wananchi kuhakikisha taarifa za wageni wanaoingia katika maeneo yao zinajulikana na, inapobidi, zinawasilishwa kwa vyombo husika vya usalama. Hii itasaidia kulinda amani, usalama na utulivu wa maeneo yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia uwezekano wa watu wenye nia ovu kujificha ndani ya jamii na kusababisha changamoto za kiusalama.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na mshikamano uliopo nchini, akisema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa utulivu kutokana na umoja na upendo wa wananchi wake.

“Tanzania yetu haigawanyiki Mungu alivyotupa nchi hii, na kama ambavyo nyinyi watu wa Babati mmepewa ardhi hii kuwa makazi yenu, basi mna wajibu wa kuilinda. Hapa ni nyumbani kwenu, msikubali mtu yeyote aje kucheza na utulivu wa maeneo yenu,” amesema.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...