-Masoko ya Kaboni Kufungua Fursa Mpya za Ajira na Uwekezaji


Na Chalila Kibuda,Michuzi TV

Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kimesema kuwa mustakabali wa ajenda ya mabadiliko ya tabianchi na uchumi wa kijani nchini unategemea nguvu, ubunifu na uongozi wa vijana, huku kikihimiza ushiriki wao katika kutumia fursa zinazotokana na sekta hiyo inayokua kwa kasi duniani.

Akizungumza katika Mkutano wa Vijana wa mwaka 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Kathryn Kigaraba, amesema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa moja ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia, lakini pia ni miongoni mwa fursa muhimu za kiuchumi zinazoweza kuleta maendeleo makubwa kwa Tanzania.

Kathryn amesema tayari Tanzania inaendelea kushuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia mabadiliko ya mifumo ya mvua, ukame, mafuriko, uharibifu wa mifumo ikolojia pamoja na changamoto mbalimbali zinazoathiri maisha ya wananchi.

Amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka na ushiriki wa makundi yote ya jamii, hususan vijana.

Aidha, amesema dunia inaelekea katika uchumi wenye matumizi madogo ya kaboni na unaostahimili athari za Mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo tayari limeanza kuzalisha mamilioni ya ajira na kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola katika sekta za nishati jadidifu, kilimo himilivu, teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, urejeshaji wa misitu, masoko ya kaboni, fedha za Mabadiliko ya tabianchi pamoja na usimamizi wa taka.

Kathryn amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kutokana na fursa hizo kwa kuwa na rasilimali nyingi za asili zikiwemo misitu ya miombo, maeneo ya mikoko, maeneo ya kilimo na bioanuwai yenye uwezo mkubwa wa kuvutia uwekezaji katika miradi ya kaboni na hatua nyingine za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Vijana ndiyo kundi kubwa zaidi la wananchi nchini. Ni wabunifu, wajasiriamali, watafiti na viongozi wa baadaye wenye uwezo wa kuongoza mageuzi ya uchumi wa kijani. Hatupaswi kuwaona kama wanufaika pekee wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bali wawe viongozi wa mabadiliko hayo,” amesema.

Amesema NCMC inalenga kuona vijana wa Tanzania wakijitokeza kuwa wataalamu wa masoko ya kaboni, wabunifu wa nishati jadidifu, wataalamu wa fedha za Mabadiliko ya tabianchi, wataalamu wa mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), wataalamu wa ufuatiliaji wa mazingira kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na wabunifu wa suluhisho za kidijitali za kufuatilia na kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, amewataka vijana kuzingatia maeneo matatu muhimu ambayo ni ubunifu, ujasiriamali na uongozi ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa za uchumi wa kijani.

Amesema ubunifu katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, akili mnemba, mifumo ya ufuatiliaji wa mazingira na nishati safi utakuwa muhimu katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuijenga Tanzania ya baadaye yenye ustahimilivu.

Pia amesisitiza umuhimu wa vijana kuanzisha biashara katika maeneo ya upandaji miti, nishati safi za kupikia, urejelezaji wa taka, kilimo endelevu, huduma za mazingira pamoja na maendeleo ya miradi ya kaboni, akieleza kuwa uchumi wa kijani una uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.

Amesema kuna umuhimu kwa vijana kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii, kushiriki katika utungaji wa sera na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia Mkataba wa Paris, Michango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDCs), mifumo ya masoko ya kaboni pamoja na mipango mingine ya maendeleo endelevu.

Ameongeza kuwa NCMC itaendelea kusaidia juhudi hizo kupitia uhamasishaji wa uanzishaji wa miradi ya kaboni, mifumo ya ufuatiliaji, taarifa na uthibitishaji wa takwimu za kaboni (MRV), uhamasishaji wa fedha za Mabadiliko ya tabianchi, tafiti, ubunifu pamoja na kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali.

Aidha, amesema vijana wanapaswa kujifunza ujuzi mpya na kutumia fursa zinazopatikana katika masoko ya kaboni, nishati jadidifu, kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira ili wawe sehemu ya kujenga Tanzania yenye ustahimilivu na maendeleo endelevu.

“Msisubiri mustakabali uje wenyewe. Uundeni, uongozeni na umilikini. Kwa pamoja tunaweza kubadili ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kuwa chanzo cha fursa za uchumi wa kijani na kujenga Tanzania yenye ustawi kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.


Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Kathryn Kigaraba akizungumza katika Mkutano wa Vijana wa mwaka 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam kuhusiana  mabadiliko ya tabianchi na fursa katika ya masoko ya Kaboni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...