Uongozi wa Kituo cha Afya Ilazo umefanya kikao cha watumishi wote kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026 kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu, kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Kikao hicho kiliongozwa na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ilazo, Dr. Mathei Kauki na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wageni waalikwa, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Kituo, Nkinda Shekilaghe na Afisa Utumishi wa Jiji la Dodoma, Steven Senguo.

Akizungumza katika kikao hicho, Dr. Kauki aliwapongeza watumishi kwa juhudi kubwa wanazoendelea kuzionesha katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza bidii, nidhamu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Jiji la Dodoma, Steven Senguo aliwakumbusha watumishi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kushirikiana kwa karibu ili kufikia malengo ya taasisi pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Kituo hicho, Nkinda Shekilaghe alieleza kuwa ushirikiano kati ya watumishi na viongozi ni msingi muhimu wa mafanikio ya kituo hicho, akihimiza kuendelea kudumisha mshikamano na kujenga mazingira bora ya kazi.

Katika hatua ya kuthamini utendaji kazi, uongozi wa Kituo cha Afya Ilazo ulitoa zawadi na vyeti kwa watumishi pamoja na vitengo vilivyofanya vizuri zaidi katika kipindi hicho. Vitengo vilivyotambuliwa ni pamoja na Kitengo cha Maabara, Kitengo cha RCH (Afya ya Mama na Mtoto) na Kitengo cha Famasi.

Kituo cha Afya Ilazo kinaendelea kutekeleza dhamira yake ya kutoa huduma bora, salama na zenye kuzingatia mahitaji ya jamii.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...