Na Mwandishi Wetu.
WAKULIMA wa zao la miwa katika wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro wamehimizwa kutumia viuatilifu kwa usahihi na kufuata taratibu za usalama ili kujikinga na madhara yanayoweza kuathiri afya zao pamoja na mazingira.
Rai hiyo imetolewa na Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Kibaha, Ngabo Vicent Pamba wakati wa mafunzo maalumu yaliyofanyika eneo la Mtibwa wilayani Mvomero, yakihusisha wakulima wa miwa, maafisa ugani, wauzaji wa pembejeo za kilimo pamoja na maafisa wa mazingira.
Ngabo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao la miwa kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu na namna salama ya kuhifadhi na kutupa vifungashio vya viuatilifu baada ya matumizi.
“Tuko hapa kutoa mafunzo mahususi kwa wakulima, maafisa ugani, wauzaji wa pembejeo na maafisa wa mazingira kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na uhifadhi salama wa vifungashio vyake. Lengo ni kuiepusha jamii ya wakulima na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu,” amesema Ngabo.
Ameeleza TARI Kibaha imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za kuboresha kilimo cha miwa nchini na kwamba mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija huku wakilinda afya zao na mazingira.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha za kutosha kusaidia utekelezaji wa programu zinazolenga kuimarisha usalama wa wakulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Raphael Mwezi, amesema mamlaka hiyo imeungana na TARI katika kutoa elimu kwa wakulima ili kuhakikisha matumizi ya viuatilifu yanafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
“Hili ni jukumu letu la kisheria kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kujikinga dhidi ya madhara ya viuatilifu. Tumekuwa tukitoa mafunzo katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Mvomero na sasa tunaendelea kufikia maeneo mengine ya Kilosa ili kuhakikisha wakulima wengi zaidi wananufaika,” amesema Mwezi.
Naye Ofisa Kilimo wa Mtibwa, Lucas Mtoi, amepongeza TARI Kibaha kwa kuandaa mafunzo hayo akisema yamekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima na wataalamu wa kilimo katika eneo hilo.
“Mafunzo haya yamewasaidia wakulima kuelewa umuhimu wa kutumia vifaa kinga na kufuata maelekezo ya matumizi ya viuatilifu ili kulinda afya zao na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema Mtoi.
Baadhi ya wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuitumia kuboresha shughuli zao za uzalishaji wa miwa.
Mkulima kutoka kijiji cha Luhungo, Kata ya Mtibwa, Elikunda Emmanuel Wanjama, amesema mafunzo hayo yamefungua uelewa wake kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu na namna ya kujikinga dhidi ya madhara yake.




.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...