Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Watanzania wataanza kushuhudia kushuka kwa bei za mafuta kuanzia mwezi Julai mwaka huu kufuatia kuanza kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia baada ya kusitishwa kwa mapigano ya Mashariki ya Kati.
Akijibu mwongozo wa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, Bungeni jijini Dodoma leo, Juni 26, 2026, Waziri Ndejembi amesema Serikali imezielekeza EWURA, TPDC na PBPA kuhakikisha manufaa ya kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia yanawafikia walaji nchini.
Amesema licha ya athari za vita kati ya Iran, Israel na Marekani zilizosababisha usumbufu katika usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, Tanzania iliendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta bila kukumbwa na uhaba.
Ndejembi amesema hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali zilihakikisha mafuta yanapatikana katika maeneo yote ya nchi, huku Tanzania ikiendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye bei nafuu za mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameeleza kuwa baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano, bei ya mafuta ghafi imeanza kushuka hadi kufikia takribani dola 70 kwa pipa, hali inayotarajiwa kuleta nafuu katika soko la ndani kadri shehena mpya zilizonunuliwa kwa bei ya chini zitakavyoingia nchini.
“Watanzania wataanza kuona punguzo la bei kuanzia mwezi Julai, na kadri shehena mpya za mafuta zilizonunuliwa kwa bei nafuu zitakavyoendelea kuwasili nchini, ndivyo bei zitakavyozidi kushuka,” amesema Waziri Ndejembi.
Aidha, amesema wataalamu wa soko la dunia wanatarajia ndani ya wiki nane hadi 10 bei za mafuta kurejea katika viwango vilivyokuwepo kabla ya kuanza kwa mgogoro huo mwezi Februari mwaka huu.
Waziri Ndejembi ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia huku ikiimarisha mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini, ikiwemo kuongeza vyanzo vya uagizaji wa mafuta na kuharakisha utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta mkoani Tanga ili kuimarisha usalama wa nishati nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...