RABIA: CCM INATHAMINI JASHO LA KILA MTANZANIA.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndg. Rabia Abdalla Hamid amesema Chama cha Mapinduzi kinathamini sana jasho la kila Mtanzania.
Amesema CCM kupitia Serikali yake imejipanga kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanagusa na kufikiwa kwa namna moja ama nyingine, ili yaweze kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za kujiletea maendeleo.
Akizungumza Juni 14, 2026 mkoani Lindi alipokutana na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, vyama vya ushirika, baba lishe na mama lishe, maafisa usafirishaji, wajane, watu wenye mahitaji maalum, viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wastaafu pamoja na vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.
“Ndugu zangu Wanalindi, CCM inatambua jasho lenu katika kujitafutia mali kupitia shughuli zenu mbalimbali kama kilimo, biashara na ujasiriamali, Serikali ya CCM itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili mnufaike na shughuli zenu”.
Aidha, ameyaomba makundi hayo kuendelea kushirikiana na CCM kwa ukaribu zaidi, kutoa ushauri na mawazo yatakayojenga umoja na mshikamano, ili kuendelea kuisimamia Serikali kwa ukaribu zaidi.
Amesema Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha tabasamu la kweli kwa kila Mtanzania na kwa makundi yote ya kijamii.
Amesema anahitaji kuungwa mkono na kutiwa moyo katika kuhakikisha anaendelea kuliongoza Taifa kwa kuliletea maendeleo yatakayogusa makundi yote, pia katika mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali 2026/2027, Serikali imekusudia kutenga asilimia 15 ya mapato ya halmashauri kutoka asilimia 10 ya awali ili kuongeza wigo katika upatikanaji wa mikopo.
Katika hatua nyingine, Ndg. Rabia ameisihi Serikali ya Mkoa wa Lindi na uongozi wa Chama kutenga muda na kufanya mikutano maalum ya kuyasikiliza makundi ya kijamii.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...