Na Said Mwishehe,Michuzi TV

RAIS wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, amesema kwamba ndoto ya Tanzania kufikia uchumi wa thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 inategemea utekelezaji wa haraka wa mageuzi katika elimu, nishati ya umeme na utawala wa serikali.

Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa mhadhara wa wazi uliondaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Taasisi ya Uongozi pamoja na chuo hicho Rais Tharman amesema ukuaji wa taifa unategemea kujenga rasilimali watu imara na kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa shuleni inaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amebainisha Afrika inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya idadi ya watu. Kwa kuwa mamia ya mamilioni ya vijana wanatarajiwa kuingia kwenye soko la ajira katika kipindi kijacho, uundaji wa nafasi za kazi ni jambo la dharura.

Aidha amesema mwenendo wa sasa unaweza kusababisha pengo kubwa kati ya wanaotafuta ajira na nafasi za kazi zinazopatikana.“Hili si pengo la idadi pekee, bali ni pengo la matumaini na fursa.”

Ili kutatua changamoto hiyo, amesema pia shule zinapaswa kuacha kuzingatia vyeti pekee na badala yake kujikita katika ujuzi wa vitendo, ushirikiano wa kikazi na kujifunza kwa maisha yote.

Ametoa mwito wa kuongeza uwekezaji katika elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi (TVET) ili kupunguza tofauti kubwa ya ujuzi unaohitajika na unaopatikana.

Rais Tharman ameongeza mafunzo ya ujuzi yanapaswa kuunganishwa moja kwa moja na maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa teknolojia ya kidijitali na sera za biashara ili kusaidia sekta binafsi kuzalisha ajira.

Kuhusu nishati, Tharman amesema kuwa umeme ndiyo injini kuu ya maendeleo ya viwanda na kufafanua upatikanaji hafifu wa umeme bado ni kikwazo kikubwa kwa mataifa mengi ya Afrika.

Ametumia nafasi hiyo kuihimiza Tanzania kuhamia kwenye nishati safi ili kuimarisha mifumo ya umeme, kuvutia wawekezaji wa kimataifa na kupunguza utegemezi wa mifumo ya zamani yenye gharama kubwa.

Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga na kuboresha njia za usafirishaji wa umeme na miundombinu ya gridi za taifa.

Kuhusu biashara, Tharman alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA). Alisema kuwa mgawanyiko wa masoko unaathiri ukuaji wa kampuni za ndani.

Alieleza kuwa soko la pamoja lingeziwezesha biashara za Tanzania kupanuka zaidi katika sekta za viwanda, kilimo na huduma.Pia utawala bora na sheria zinazotabirika ni muhimu katika kuvutia uwekezaji wa muda mrefu kutoka nje ya nchi.

Akirejea takwimu za IMF, amebainisha kuwa kupunguza rushwa na kuongeza uwazi kunaweza kuchochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara hiyo ni hatua muhimu inayoonyesha kuimarika kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.“Mafanikio ya Singapore yanatoa mafunzo muhimu kuhusu nidhamu na mipango ya muda mrefu.”

Wakati huo huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema chuo hicho kinajivunia kuwa mwenyeji wa hotuba hiyo, akisisitiza mchango wake katika kuwaandaa vijana kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameongeza kuwa mafanikio ya Singapore yanaonyesha kwamba maendeleo yanatokana na uongozi bora na taasisi imara, si rasilimali za asili pekee.

Alihitimisha kwa kueleza kuwa mustakabali wa Afrika unategemea ubunifu wa ndani na utawala bora imara.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...