Na Janeth Raphael MichuziTv

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa, amesema Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 ni ya kipekee kwa kuwa ndiyo bajeti ya kwanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025.

Akizungumza jijini Dodoma Juni 10, 2026, amesema bajeti hiyo inalenga kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Balozi Mussa amesema kabla ya kuwasilisha bajeti hiyo bungeni Juni 11, 2026, Bunge litapokea taarifa ya hali ya uchumi wa mwaka 2025 na mwelekeo wake kwa mwaka 2026. Taarifa hiyo itaeleza mwenendo wa uchumi mkuu wa nchi ikiwemo ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), mfumuko wa bei, biashara ya nje na kiwango cha akiba ya fedha za kigeni.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inapanga kutumia Shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, ambapo fedha nyingi zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na huduma muhimu kwa wananchi. Matumizi hayo yanatarajiwa kufadhiliwa kwa kiasi kikubwa na mapato ya ndani yatakayofikia Shilingi trilioni 46.8, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia maendeleo yake.

Amesema miradi ya kimkakati itakayopewa kipaumbele ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa miundombinu ya barabara, miradi ya maji, nishati pamoja na maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi. Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kufikia malengo yaliyowekwa katika mwaka wa fedha 2025/26.

Kuhusu maboresho ya kodi, ada na tozo, Waziri Mussa alisema Serikali ilipokea mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za Serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara, taasisi za elimu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi. Kati ya hayo, mapendekezo 125 yalikubaliwa moja kwa moja, 121 yaliboreshwa na kukubaliwa huku 295 yakikataliwa, na mengine kupelekwa kwa uchambuzi zaidi.

Amesema ushirikishwaji wa wadau pamoja na ushauri wa Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi na kamati ya kiufundi ya “Think Tank” umesaidia kupata mawazo yatakayoboa mfumo wa kodi, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Aliwataka Watanzania kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kufuatilia kwa karibu uwasilishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 utakaofanyika bungeni Juni 11, 2026.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...