Farida Mangube, Morogoro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imezindua jengo jipya la Ofisi ya Mkoa wa Morogoro lililogharimu Shilingi bilioni 1.63, huku ikitoa wito kwa wananchi kuongeza ushiriki katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma inaonekana na mianya ya rushwa inazibwa.

Akizindua jengo hilo Juni 1, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ujenzi wa ofisi za taasisi hiyo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Amesema Serikali imeendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha za kujenga miundombinu ya kisasa, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kwa idadi ya majengo yanayojengwa na yaliyokwishajengwa, ni wazi kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuimarisha taasisi hii. Huu ni ushahidi wa dhamira yake ya kuendelea kupambana na rushwa nchini,” amesema Chalamila.

Amebainisha kuwa TAKUKURU ina jumla ya ofisi 145 nchini, zikiwemo ofisi za mikoa 28, wilaya 111 na vituo maalumu sita. Hata hivyo, kati ya hizo, ni ofisi 70 pekee zinazomilikiwa na taasisi hiyo, huku ofisi 64 zikiendelea kutumia majengo yasiyomilikiwa na TAKUKURU.

Kwa mujibu wa Mkuu wa huyo wa TAKUKURU, katika mwaka wa fedha 2025/2026 taasisi hiyo inaendelea kujenga majengo 11 mapya, likiwemo jengo moja la mkoa na majengo 10 ya wilaya.

“Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyobahatika kufikiwa mapema katika mpango huu wa ujenzi wa majengo ya kudumu ya TAKUKURU,” aMEsema.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Usimamizi wa Milki wa TAKUKURU, Dkt. Emmanuel Kiyabo, amesema mradi huo ulitekelezwa kwa gharama ya Shilingi 1,627,857,615.81, ikiwa ni ongezeko la Shilingi milioni 27.8 kutoka bajeti ya awali ya Shilingi bilioni 1.6.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo la asilimia 1.74 lilitokana na maboresho ya kiufundi yaliyofanyika wakati wa utekelezaji wa mradi, ikiwemo kuongeza mota za kufungua na kufunga mageti yote mawili ya uzio, kuongeza eneo la paving blocks na kazi za kuboresha eneo la kuingilia kutoka barabarani.

Dkt. Kiyabo amesema mradi ulianza Machi 6, 2025 na ulitarajiwa kukamilika Januari 5, 2026, lakini ulikamilika Machi 30, 2026 baada ya kuchelewa kwa takribani miezi mitatu.

Alitaja sababu za kuchelewa kwa mradi kuwa ni uhaba wa mabati ya kuezekea, kuchelewa kupatikana kwa vifaa vya ukuta wa vioo, mvua za masika pamoja na kusitishwa kwa baadhi ya shughuli kufuatia mazingira yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mradi huo ulitekelezwa kwa mfumo wa Design and Build kupitia ushirikiano kati ya TAKUKURU na Shirika la Magereza (PCS), ambapo wataalamu kutoka taasisi hizo walihusika katika usanifu, usimamizi na utekelezaji wa kazi za ujenzi.

Jengo hilo limejengwa katika eneo la Kihonda Kilimanjaro Manispaa ya Morogoro na linajumuisha jengo kuu la ofisi lenye ghorofa moja, nyumba ya walinzi, nyumba ya jenereta na miundombinu mingine ikiwemo tenki la maji la lita 60,000, mnara wa matenki ya maji, uzio wa kisasa na eneo la maegesho na bustani.

Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amewataka watumishi wa TAKUKURU kuyatunza majengo mapya yanayojengwa na Serikali ili yaweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na TAKUKURU katika kusimamia matumizi ya fedha za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alisema halmashauri zinapaswa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za miradi inayotekelezwa pamoja na fedha zinazotumika ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.

“Ni muhimu wananchi wakafahamu miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kushiriki kuifuatilia. Hii itasaidia kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na kuzuia mianya ya rushwa,” alisema.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu dhidi ya rushwa kwa vijana kupitia Klabu za Wapinga Rushwa shuleni, akieleza kuwa kujenga kizazi kinachochukia rushwa ni msingi muhimu wa mafanikio ya mapambano hayo kwa siku zijazo.

Uzinduzi wa jengo hilo ulihudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Kamati ya Usalama ya Mkoa, watumishi wa TAKUKURU, wanafunzi wa Klabu za Wapinga Rushwa pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...