Na Atley Kuni, WAF-Dar es Salaam
Washiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Kinywa na Meno Tanzania kutoka Mataifa mbalimbali duniani wameisifu Tanzania kwa ukarimu, mapokezi mazuri na ushirikiano wa hali ya juu walioupata katika kipindi chote cha maonesho hayo yaliyofanyika nchini.
Washiriki hao wamesema mazingira rafiki yaliyoandaliwa yamechangia mafanikio makubwa ya maonesho na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kibiashara kwa sekta ya afya ya kinywa na meno.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Ndugu Emmanuel Tayari, amesema mafanikio ya maonesho hayo yanaonesha nafasi ya Tanzania kama kitovu muhimu cha uwekezaji, ubunifu na ushirikiano kwenye huduma za afya barani Afrika, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea maendeleo ya sekta hiyo.
Washiriki kutoka nje ya nchi wameelezea Tanzania kuwa ni taifa lenye watu wenye upendo, heshima na wanaozingatia misingi ya kidiplomasia, jambo ambalo limewavutia wengi wa wageni hao,wengi wameahidi kurejea Tanzania kushiriki katika maonesho yajayo.
"Maonesho haya yametupatia fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza teknolojia mpya zinazolenga kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno kwa wananchi" amesema Mshiriki Mmoja kutoka nchini Zambia.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, afya bora ya kinywa na meno ni sehemu muhimu ya afya kwa ujumla kwani huchangia kuzuia magonjwa mbalimbali na kuboresha ustawi wa maisha ya jamii.
Naibu Katibu Mkuu Bw. Tayari amewahakikishia washiriki ushirikiano wa karibu kutoka Serikali kwa maandalizi ya maonesho yajayo yatakayofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Mei, 2027.
"Serikali itaendelea kurahisisha taratibu za uingizaji wa bidhaa za kinywa na meno zitakazotumika katika maonesho hayo ili kuhakikisha washiriki wanapata mazingira bora ya kushiriki na kuonesha ubunifu wao", amesema Tayari.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu Tayari amewataka, washiriki hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuwahamasisha watengenezaji na wadau wengine wa bidhaa za kinywa na meno kutoka mataifa mbalimbali kushiriki kwa wingi katika maonesho yajayo. Hatua inayo tarajiwa kuongeza uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuendelea kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.



.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...