Jumla ya wahatimu 440 waliokuwa wanachama wa club za kodi, kutoka vyuo  vinne vya UDOM, CBE, Mipango na St. John’s, wamefanya mahafali kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha St. John’s, jijini Dodoma, huku wakitakiwa kutumia elimu waliyoipata kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika mahafali hayo Juni 13, 2026, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma, Pendolake Elinisafi, amesema Klabu za Kodi ni jukwaa muhimu la kuwajengea vijana uelewa kuhusu umuhimu wa kodi na mchango wake katika maendeleo ya nchi, amebainisha kuwa vijana wa leo ndio walipakodi wa kesho, hivyo wanapaswa kuandaliwa mapema kuwa raia wenye uelewa wa masuala ya kodi.

Elinisafi amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania, ilianzisha Klabu za Kodi mwaka 2018 katika shule za sekondari na vyuo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha elimu ya kodi kwa vijana na kujenga kizazi kitakachozingatia ulipaji wa kodi kwa hiari, ameongeza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa kuepuka mtazamo hasi dhidi ya kodi na kuanzisha biashara zinazofuata sheria za kodi.

Alieleza kuwa maendeleo mengi yanayoonekana nchini yanatokana na mapato ya ndani yanayokusanywa kupitia kodi, ikiwemo utoaji wa elimu bila malipo, mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, uboreshaji wa miundombinu, ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR), madaraja na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Elinisafi aliwataka wasimamizi wa Klabu za Kodi kuendelea kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kujiunga na klabu hizo na viongozi wa klabu kuwaalika maafisa wa TRA katika mijadala mbalimbali ya wanafunzi ili kuendelea kupata elimu sahihi ya kodi, huku akiwatakia wahitimu maisha mema baada ya masomo yao na kuwataka waendelee kuwa mabalozi wazuri wa elimu ya kodi popote watakapokuwa.

Kwa niaba ya wahitimu, viongozi wa Klabu za Kodi wameishukuru TRA kwa mafunzo na elimu waliyoipata, wakisema imewajengea uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya taifa, wakiahidi kuwa mabalozi wazuri  kwa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...