Na Said Mwishehe,Michuzi TV


RAIS wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akiwa nchini Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kufanya mazungumzo ya uwili na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye manufaa kwa Wananchi wa Tanzania na Namibia.

Pia Rais Ndaitwah na mwenyeji wake Rais Dk.Samia wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa hati mbalimbali za makubaliano ya ushirikiano kati ya Nchi hizo mbili.

Aidha pamoja na mambo mengine inaelezwa kwamba ziara hiyo inakwenda kufungua fursa zaidi za kiuchumi kati ya nchi hizo ambazo zimekuwa na urafiki wa kindugu na wa kihistoria kwa muda mrefu.

Akizungumzia ziara hiyo alipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya Rais Ndaitwah, Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Caesar Waitara, amesema ziara hiyo ni ishara ya uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria uliopo kati ya mataifa hayo mawili, huku akisisitiza kuwa ziara hiyo inaleta manufaa makubwa katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Balozi Waitara anasema Rais wa Namibia anaitazama Tanzania kama nyumbani kwake kutokana na historia yake ya kuishi nchini kwa miaka sita alipokuwa mwakilishi wa chama cha SWAPO katika nchi za Afrika Mashariki.

Anabainisha kuwa makao yake yalikuwa katika eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam, jambo linaloimarisha zaidi uhusiano wake binafsi na Tanzania.

“Ujio wake unaonyesha jinsi uhusiano kati ya Tanzania na Namibia ulivyo imara na wa muda mrefu. Kila mara anapokuja Tanzania anajisikia kama yuko nyumbani,” anasema Waitara.

Anaeleza kuwa Namibia inaendelea kuthamini mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa taifa hilo, hususan kupitia kambi za wapigania uhuru zilizokuwa Kongwa pamoja na msaada wa mafunzo ya kijeshi uliotolewa kwa wapigania uhuru wa Namibia.

Kwa mujibu wa balozi huyo, pamoja na historia ya ukombozi, mataifa hayo sasa yamejikita zaidi katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji na kubadilishana uzoefu katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Waitara anasema Tanzania inaendelea kusukuma mbele ajenda ya diplomasia ya uchumi kupitia balozi zake nje ya nchi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kufungua fursa za biashara.

Anataja uwekezaji wa Watanzania nchini Namibia kuwa ni mfano wa mafanikio ya ushirikiano huo, ambapo baadhi ya Watanzania wameanzisha biashara na taasisi za elimu.

Anabainisha kuwa kuna chuo kikuu nchini Namibia kinachomilikiwa kwa asilimia 100 na Mtanzania, ambacho kinatoa elimu ya shahada, shahada za uzamili na uzamivu, huku kikiwa na zaidi ya wanafunzi 10,000.

Aidha, Watanzania wengine wanaendelea kufanya biashara mbalimbali nchini humo, wakati WanaNamibia wamewekeza Tanzania katika sekta za utalii na mawasiliano.

Katika kuimarisha mahusiano ya kitamaduni, Waitara anasema ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) umeanza kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa njia ya mtandao nchini Namibia.

Anafafanua wanafunzi 26 walihitimu mafunzo ya awali mwaka jana, huku kundi jipya la wanafunzi 40 likitarajiwa kuanza masomo hivi karibuni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akizungumzia ziara ya Rais wa Namibia anasisitiza ni uthibitisho kuwa mahusiano ya kihistoria kati ya mataifa hayo sasa yamepanuka na kuwa ushirikiano mkubwa wa kiuchumi.

Anasema maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yanaifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi nyingi za ukanda wa Kusini mwa Afrika, jambo linaloweza kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Namibia.

Wakati Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, anasema mafanikio ya diplomasia ya uchumi hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa usalama.

Ananasisitiza kuwa amani na utulivu wa Tanzania ndiyo msingi unaowezesha viongozi wa kimataifa kutembelea nchi na wawekezaji kuendelea kuwekeza.

“Usalama ni mtaji muhimu wa uchumi. Bila usalama hakuna biashara, hakuna uwekezaji wala maendeleo. Ni jukumu la kila mwananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi yetu,” anasema Kamanda Muliro.

Ziara ya Rais wa Namibia nchini Tanzania inatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kihistoria, kiuchumi na kitamaduni kati ya mataifa hayo mawili, huku ikifungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...