KUTOKA VUNJO
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Enock amewahimiza vijana kuendelea kumcha Mungu, kuzingatia maadili mema na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.
Koola alitoa kauli hiyo leo wakati wa ufunguzi wa bonanza la michezo la vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Kilimanjaro mashariki lililofanyika Marangu mashariki lililowakutanisha vijana 500 kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Koola aliwasisitiza vijana kujiepusha na makundi ya kihalifu, kuwa wazalendo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii na taifa.
Bonanza hilo linalenga kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa vijana kupitia ibada, maombi, kujifunza Neno la Mungu na kushiriki michezo mbalimbali inayokuza afya, nidhamu na maendeleo ya kijamii.
Alieleza kuwa, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi ambapo zinajumuisha mafunzo ya ufugaji wa kuku wa kibiashara, ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, ufugaji wa samaki, kilimo cha kisasa na ujasiriamali, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuongeza kipato.
Alisema kuwa, ofisi yake imewaajiri vijana mahsusi ili kuwasaidia wenzao kuunda vikundi vya kiuchumi, kuandaa katiba za vikundi, kukamilisha nyaraka za maombi ya mikopo ya Halmashauri isiyo na riba, pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu.
Alisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ni msingi wa maendeleo endelevu ya Jimbo la Vunjo na Taifa kwa ujumla na kuahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za dini na wadau mbalimbali katika kuwawezesha vijana kupata elimu, stadi za maisha na fursa za kiuchumi zitakazowasaidia kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya nchi.



.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...