Na Mwandishi Wetu, Tabora

Wananchi wa mikoa ya Tabora na Katavi wameanza kushuhudia matokeo ya Mradi Shirikishi wa Uhifadhi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame, huku shughuli za uhifadhi zikigeuka kuwa chanzo cha kipato, ajira na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Mafanikio hayo yamebainika wakati Kamati ya Wataalamu ya mradi ilipofanya ziara ya Julai 15 na 16, 2026 kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika maeneo ya mradi na kujionea namna zinavyowanufaisha wananchi.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora kabla ya ziara hiyo, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Dk. Zainabu Bungwa, alisema mradi umeanza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika uhifadhi wa misitu na ustawi wa jamii kupitia uwekezaji kwenye shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Alisema mradi umewezesha uanzishwaji wa vikundi vya wananchi vinavyojishughulisha na shughuli za kiuchumi, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa magari na pikipiki kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali za misitu, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mbegu za miti, mashamba darasa ya kilimo mseto cha misitu, ufugaji wa nyuki, maeneo ya malisho ya mifugo pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tunaanza kuona matokeo chanya ya mradi katika maeneo mengi. Wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye shughuli za uhifadhi huku wakiongeza kipato kupitia fursa zinazotokana na matumizi endelevu ya misitu,” alisema Dk. Bungwa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, John Gharuth Mboya, alisema mafanikio ya mradi yanapaswa kuambatana na uelewa wa pamoja wa viongozi wa mikoa na wilaya ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake.

Alisema kuna umuhimu wa kuandaliwa taarifa ya kina itakayowasilishwa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya husika ili kuzijengea uelewa kuhusu malengo, mafanikio na mchango wa mradi katika maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Afisa Misitu wa Mkoa huo, Augustine Hildagadess, aliwataka wananchi kutenga maeneo rasmi ya malisho ya mifugo ili kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi na kuimarisha uhifadhi wa misitu.

Akizungumza baada ya kutembelea vijiji vya Mtakuja na Legezamwili wilayani Mlele, alisema wataalamu wa mradi wataendelea kushirikiana na vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi yatakayolinda mazingira na wakati huo huo kukuza uzalishaji.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Wataalamu iligawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza lilikagua shughuli za mradi wilayani Sikonge, Kituo cha Ulinzi na Kituo cha Ufugaji Nyuki cha TFS Mlele pamoja na ofisi za viongozi wa Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mlele, huku kundi la pili likitembelea shughuli zinazotekelezwa katika wilaya za Urambo na Kaliua.

Mradi Shirikishi wa Uhifadhi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani 6,785,882 unatekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2027 ukiwa na lengo la kurejesha takribani hekta 34,000 za misitu ya miombo iliyoharibiwa, kuboresha maisha ya wananchi wanaoizunguka misitu na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.

Mbali na TFS na FAO, utekelezaji wa mradi unahusisha Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), ICRAF, TARI, Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo, TAMISEMI pamoja na vikundi vya kijamii vinavyoshiriki katika shughuli za uhifadhi na maendeleo kwenye maeneo ya mradi.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...