Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itakamilisha mchakato wa kuunda Halmashauri ya Mwibara ili kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.

Ametoa kauli hiyo leo Julai 4, 2026, alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, baada ya Mbunge wa Bunda Vijijini, Mhe. Boniface Mwita Getere, kuwasilisha ombi la wananchi la kuanzishwa kwa halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu alisema Serikali imepokea hoja hiyo na kutambua umuhimu wake, akibainisha kuwa utaratibu wa kuanzisha halmashauri mpya utaendelea kufuatwa ili kuhakikisha huduma za Serikali zinawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

"Nimeipokea hoja hii. Serikali ina utaratibu unaofuatwa katika kugawa maeneo ya kiutawala. Nimemuelekeza Mkuu wa Mkoa pamoja na Sekretarieti ya Mkoa kuendelea na mchakato huo ili Serikali iweze kupeleka mapendekezo kwenye mamlaka husika kwa hatua zinazostahili," alisema Waziri Mkuu.

Alisema Serikali imeendelea kutekeleza sera ya kusogeza huduma karibu na wananchi, ndiyo sababu imekuwa ikiendelea kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala pale inapobainika kuwa kuna uhitaji wa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Katika kufafanua hatua za utekelezaji wa Serikali, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alisema Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma katika Wilaya ya Bunda kupitia uwekezaji katika sekta za afya, elimu na miundombinu, huku ikikamilisha hospitali, vituo vya afya na kuongeza watumishi wa sekta ya afya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, alisema Serikali itaendelea na mpango wa kupanga matumizi bora ya ardhi na kupima vijiji, sambamba na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ardhi ili kudhibiti migogoro ya umiliki na kuhakikisha hati mbili hazitolewi katika eneo moja.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, alisema Serikali itaendelea kukamilisha Mradi wa Maji wa Onyamswa pamoja na miradi mingine ya maji katika Bunda, akisisitiza kuwa kipaumbele ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kabla ya ujenzi wa miundombinu ya utawala.

Aidha, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Mara, huku wananchi wa maeneo ya mijini yenye sifa za vijijini wakiendelea kunufaika na utaratibu wa kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utawala bora na kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia uanzishwaji wa maeneo mapya ya kiutawala pale inapobainika kuwa kuna uhitaji, sambamba na kuendelea kuwekeza katika sekta za afya, elimu, maji, nishati na miundombinu ya maendeleo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...