-Asema mijadala iko huru kwa wabunge wa vyama vyote, aeleza wapinzani wanavyopewa nafasi

-Pia azungumzia maandalizi kuelekea historia miaka 100 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano




Na Said Mwishehe,Michuzi TV


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amevunja ukimya huku akiwazodoa wale wanadai Bunge ni dhaifu na halina meno.

Kutokana na hali hiyo, amesema kuwa Bunge lililopo na yake yaliyopita hakuna lililo dhaifu kwani kazi kubwa inayofanyika ni kuisimamia Serikali pamoja na kuwawakilisha wananchi ikiwamo kutunga sheria mbalimbali pamoja na kusimamia ustawi wa jamii.

Akizungumza katika kikao kati yake na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu miaka 100 ya historia ya Bunge, ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa nyakati zote likiwamo Bunge analoliongoza bado anatoa uwanja sawa kwa wabunge wa upinzani picha ya uchache wao.

Aidha amesema na kuhoji kuwa mjadala wa Bunge kuonekana dhaifu lakini nyakati zote bado wabunge wa upinzani wamekuwa wakipewa haki sawa kama takwa la kidemokrasia linavyotaka.

“Ndugu zangu kuna mambo yanaendelea na kuibuliwa na baadhi ya vyama vya upinzani. Kumbukeni mwaka 2015 Katiba ilikuwa ileile ambapo wabunge wa upinzani walikuwa 102 ambapo kati ya hao Chadema walikuwa 69.

“Tena wakati wanashinda Tume ya Uchaguzi kwa wakati ule haikuwa na maboresho na kambi rasmi ya upinzani ikatambulika.

“… kwanini Bunge lile lilikuwa na nguvu, lakini nini maana yake mjadala hapa chama kimoja (hakutaja jina) chama kimoja kilipata mgombea toka CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015 jambo lililowasaidia kuimarika zaidi na kupata wabunge wengi. Sasa wapo wapinzani lakini hawajaimarika.

“Hapa Dar es Salaam wapinzani waliweza kuongoza Halmashauri za Kinondoni, Ubungo na hata Ilala pia ambazo zilikuwa upinzani na hata kufikia baadhi yao kusema wapewe nafasi ili tuongoze,” amesema Spika Bunge

Ameongeza kazi ya Bunge ambayo inafanyika kwa miaka yote kwanza kuisimamia ustawi wa wananchi, kuisimamia Serikali pamoja na kitunga sheria jambo ambalo linaendelea kufanyika hadi sasa.

Katika kujenga hoja yake kuhusu Bunge analoliongoza alisisitiza kuwa hakuna Bunge dhaifu au Bunge imara kwani Bunge lolote kazi zake zinajulikana kusimamia ustawi wa jamii.


KAMATI SAA 72 BUNGENI


Spika Zungu amesema kutokana na kutoa haki kwa wabunge na wananchi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 vyama vyote vya upinzani vimeweza kupata wabunge tisa wakati hata ukitoa hoja ili uungwe mkono lazima muwe wabunge 10 lakini upinzani wakisimama wanakuwa tisa.

“Zipo hoja nzuri huyu hapa Ado (Mbunge wa Tunduru ACT) hata akitoa hoja wanakuwa tisa wakati kanuni inataka wawe 10,” amesema.

Amefafanua licha ya hali hiyo na takwa la kikanuni lakini bado Rais Samia aliagiza kamati za Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Serikali za Mitaa (LAAC) ziongozwe na wapinzani licha ya uchache wao kama njia ya kuimarisha demokrasia.

“Ni nani asiyejua kwamba Rais Dkt Samia ndio amewarudisha nchini wapinzani wengine waliokimbia nchi kwa kuwataka warudi ili tujenge Taifa letu, haya ni mapenzi makubwa ya Rais Samia.

“Hata mnaposikia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali lakini kamati ambayo kwenye Mpira tunaita kamati ya saa 72 Kwa maana PAC na LAAC ndio wajibu wa kumwita kila aliyetajwa,” amesema.



MIAKA 100 YA BUNGE


Amesema kwa sasa Bunge lipo kwenye maandalizi ya kusheherekea miaka 100 tangu kilipoanzishwa chombo hicho wakati wa utawala wa ukoloni hadi ilipozaliwa Tanzania.

“Wapo wengine watahoji kwa nini tunawataja wakoloni lazima tuwataje ili tuone tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.

“Kauli mbiu yetu katika kutimiza miaka 100 ya Bunge ni Historia yetu,Dira yetu,” amesema Spika Zungu.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...