Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeahidi kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji wa ndani kupata masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.

Hayo aliyasema Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Dkt.Latifa Khamis wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Dkt. Latifa alisema tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo miaka 50 iliyopita, yamewezesha fursa za biashara na uwekezaji zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 129.31, jambo linalodhihirisha mchango mkubwa wa Sabasaba katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Alisema TanTrade itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wa Kitanzania wanashiriki kikamilifu katika maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, hatua itakayowapa nafasi ya kutangaza, kuuza na kupanua masoko ya bidhaa zao.

"Maonesho ya Sabasaba siyo tu sehemu ya kuonyesha bidhaa, bali ni jukwaa muhimu la kukuza ubunifu, kujenga chapa za biashara na kufungua fursa mpya za biashara katika masoko ya kikanda na kimataifa," alisema.

Dkt. Latifa aliwataka Watanzania kutumia kikamilifu jukwaa la Sabasaba kuonesha ubunifu wao, kuongeza thamani ya bidhaa na kujenga ushindani unaoweza kuzifanya bidhaa za Tanzania zikubalike zaidi katika soko la dunia.

Aidha Dkt.Latifa aliwahimiza wafanyabiashara kuwa mabalozi wa Tanzania kwa kuitangaza nchi kupitia bidhaa na huduma wanazozalisha, akibainisha kuwa ushiriki wa wageni na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali katika maonesho hayo unaifanya Sabasaba kuwa fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yanayofanyika kila mwaka katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, yameendelea kuwa maonesho makubwa zaidi ya biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, yakitoa fursa kwa wazalishaji, wawekezaji na wafanyabiashara kukutana, kubadilishana uzoefu na kuanzisha ushirikiano mpya wa kibiashara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...