Na Farida Mangube
Mtanzania Bi. Rehema Katuga kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (OCPD) ameibuka mshindi katika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Uongozi na Usimamizi la Chama cha Wataalamu wa Uandishi wa Sheria wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Association of Legislative Counsel – CALC), na kuwa mmoja wa wawakilishi wawili wa Afrika katika baraza hilo.

Baraza hilo, lenye wawakilishi wawili kutoka kila bara, lina jukumu la kusimamia na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uendeshaji wa chama hicho cha kitaaluma kinachowakutanisha wataalamu wa uandishi wa sheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Bi. Katuga aliibuka mshindi katika uchaguzi uliowahusisha wagombea wanne kutoka Afrika, wakiwemo wagombea wawili kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Namibia na yeye akiwa mwakilishi pekee kutoka Tanzania. Ushindi huo umeiwezesha Tanzania kupata nafasi ya uwakilishi katika chombo hicho muhimu cha kitaaluma.

Akizungumzia umuhimu wa CALC, Bi. Katuga alisema chama hicho ni miongoni mwa vyama vya kitaaluma vinavyosimamiwa na Jumuiya ya Madola na kina jukumu la kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa uandishi wa sheria katika nchi wanachama.

Alisema CALC inalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu hao katika kuandaa sheria bora zinazotafsiri sera za Serikali na kuendana na mageuzi mbalimbali yanayohitajika katika nchi wanachama.

Aidha, chama hicho kinahamasisha ushirikiano katika mafunzo, kubadilishana uzoefu, programu za mafunzo kwa vitendo (attachments), matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria pamoja na kuendeleza mbinu bora za taaluma hiyo.

“Lakini pia chama hiki kina Baraza la Uongozi linalojumuisha viongozi wakuu pamoja na wawakilishi kutoka mabara mbalimbali ambao ndio sisi tuliochaguliwa sasa. Kwa pamoja hushiriki katika kutoa mwelekeo na kufanya maamuzi kuhusu maendeleo ya taaluma ya uandishi wa sheria,” alisema Bi. Katuga.

Mwakilishi huyo wa Tanzania na Afrika alisema nafasi hiyo itamwezesha kuchangia kuimarisha ushirikiano wa wataalamu wa uandishi wa sheria nchini Tanzania na barani Afrika, kubadilishana maarifa na uzoefu na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola, pamoja na kujifunza na kutumia mbinu bora za kisasa katika uandishi wa sheria.

Aidha, alisema anatarajia kushiriki kikamilifu katika kuunganisha wataalamu wa uandishi wa sheria barani Afrika, kukuza taaluma hiyo na kuchangia juhudi za kuboresha ubora wa sheria kupitia uandishi wenye weledi, uwazi na ufanisi.

Kwa Tanzania, uwakilishi huo unaongeza fursa ya kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo ya taaluma ya uandishi wa sheria na kunufaika na mafunzo, programu za kujengea uwezo wataalamu wa fani hiyo, pamoja na ubadilishanaji wa teknolojia na uzoefu. Hatua hiyo inatarajiwa kuchangia kuimarisha ubora wa mchakato wa uandaaji wa sheria nchini.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa katika Mkutano Mkuu wa CALC uliofanyika tarehe 19 mwezi huu nchini Singapore.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...