KATIKA kuhakikisha vijana wanawekwa viti vya mbele katika ajenda ya uchumi Serikali  inaandaa maboresho ya kisera na kisheria yatakayowaondolea vijana wajasiriamali kikwazo cha muda mrefu cha ukosefu wa dhamana za mikopo kwa kuimarisha mfumo wa udhamini wa mikopo na kuruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Rais wa Serikali ya Jamuhuri Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya kuwatambua na kukabidhi zawadi kwa washindi wa shindano la ‘Vijana Uchumi Challenge’ Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema; Serikali inatambua kundi la vijana na kuwepo kwa Wizara maalum inayoshughulikia masuala ya vijana ni moja ya mkakati wa kuhakikisha kuelekea uchumi endelevu vijana wanakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mawazo na ubunifu yenye kutatua changamoto za kijamii na uchumi.

Amesema; Serikali inaandaa maboresho ya kisera na kisheria yatakayowaondolea vijana wajasiriamali kikwazo cha muda mrefu cha ukosefu wa dhamana ya mikopo kwa kuimarisha mfumo wa udhamini wa mikopo na kuruhusu matumizi ya dhamana zinazohamishika.

“Tunataka kuhalalisha matumizi ya dhamana zinazohamishika. Kwa mfano, mkulima au mfugaji anayetumia stakabadhi ghalani aweze kuitumia hiyo kupata mkopo wa pembejeo bila kusubiri kuuza mazao yake,” ameeleza.

Amesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tayari ina dirisha la udhamini wa mikopo kwa biashara ndogo, za kati na kubwa, ambalo linaendelea kuboreshwa na litabadilishwa kuwa taasisi maalum itakayoratibu masuala ya udhamini wa mikopo nchini.

“Tayari kuna zaidi ya shilingi Bilioni 280 kwa ajili ya jukumu hilo, na wadau wengine wameonesha nia ya kushiriki kwa kiwango cha zaidi ya dola za Marekani milioni 150. Hizi zitasaidia biashara ndogo, za kati na biashara kubwa kupata udhamini wa mikopo,” ameeleza Dkt. Nchemba.

Aidha Waziri Mkuu ameeleza kuwa;  hatua hizo zinaenda sambamba na maboresho mengine ya kisheria yaliyofanywa na Serikali, ikiwemo kuondoa sharti lililokuwa likiwazuia watanzania kuwa wakandarasi wakuu wa miradi mikubwa, hatua inayopanua fursa za ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani kundi la vijana.

Pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana Dkt. Joel Nanauka amesema; Serikali inawatambua vijana, kuwasikiliza pamoja na kuwaweka katika ajenda za maendeleo ya kitaifa ikiwemo kutoa fursa za ajira na ujasiriamali.

“Tumekusanyika ili kutambua na kusherehekea ubunifu, bidii na ujasiri wa vijana wetu katika Vijana Uchumi Challenge – Mpango ambao unalenga kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali na wabunifu katika uchumi wa Taifa, kwa kuwa tunatambua vijana ndio nguvu ya Taifa na ndio wabebaji wa maendeleo ya kesho.” Amesema.

Aidha ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwaweka vijana viti vya mbele katika agenda ya uchumi na kupitia shindano hilo vijana wamepata fursa ya kutoa maoni yao, kuwasilisha biashara zao na kuonyesha uwezo wao.

“Leo, tunawapa heshima vijana ambao wamethubutu, wamefanya kazi kwa bidii, na wameonyesha kuwa hata katika changamoto za kiuchumi, wanaweza kujenga suluhisho.” Amesema.

Aidha amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono kupitia mikopo nafuu, mafunzo, fursa za ajira na ushirikiano na sekta binafsi ili kuliinua kundi hilo muhimu katika ustawi wa Taifa kiuchumi na jamii.

Akifafanua kuhusu shindano hilo Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana Jenifa  Omolo amesema shindano la “Vijana Uchumi Challenge lililobeba kauli mbiu ya ‘Wana Tunafikiri, Taifa Linasonga’ limekuwa jukwaa muhimu na limetoa nafasi ya kuibua fikra na ubunifu wa vijana, kujenga ujasiri, na kuonyesha kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kubuni suluhisho za changamoto za kiuchumi na kijamii. 

Amesema kuwa shindano hilo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwashirikisha vijana kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. 

“Serikali inataka vijana wawe sehemu halisi ya maendeleo na kushiriki kikamilifu na si watazamaji tu.”Ameongeza.

Aidha ameeleza kuwa kabla ya mchakato wa kuwapata washindi watatu, maombi zaidi ya 7000 yalipokelewa na kuchujwa hadi kufikia vijana 100 waliopatiwa mafunzo na kusisitiza kuwa Serikali itaunda mfumo wa kuwafuatilia baada ya shindano.

“Ili mawazo yao yasibaki kwenye makabati wataunganishwa na fursa, taasisi za fedha na viongozi wa taasisi mbalimbali ili mawazo yaweze kuleta tija kwa jamii na kusaidia vijana wengine.” Aliongeza.

Katika matokeo yaliyotangazwa kwenye fainali ya shindano hilo, Jofrey Sanga ameibuka mshindi wa kwanza na kujishindia shilingi milioni 50, Jacob Fabian ameshika nafasi ya pili na kutwaa zawadi ya shilingi milioni 30, huku Robert Malonga akimalıza katika nafasi ya tatu na kujinyakulia kitita cha shilingi milioni 20 kupitia mawazo ya kibunifu yanayoweza kuchangia mandeleo ya Taifa katika kujenga uchumi imara, shindani na unaojumuisha ubunifu kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika hafla ya kuwatambua na kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la Vijana Uchumi Challenge, Nchemba amesema Serikali itaendelea kutoa fursa kwa kundi hilo katika kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.Leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana Dkt. Joel Nanauka akizungumza katika hafla hiyo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha vijana kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. Leo jijini Dar es Salaam.


Matukio mbalimbali wakati wa Hafla ya kuwatambua na kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la Vijana Uchumi Challenge, Leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...