Na Pamela Mollel,Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amemtaka Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa, kuimarisha utendaji wa shirika hilo kwa kuhakikisha sekta ya uhifadhi na utalii inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa

Akizungumza jijini Arusha wakati wa hafla ya kumuapisha Kamishna huyo, Waziri Kijaji amesema uongozi mpya unapaswa kuelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya hifadhi, kuongeza fursa za uwekezaji, kuanzisha bidhaa mpya za utalii na kusimamia mapato kwa ufanisi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa nchi

Pia alisisitiza umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, akieleza kuwa ushirikiano wao ni nguzo muhimu katika kulinda rasilimali za taifa

Aidha, alimwelekeza Kamishna kuhakikisha nidhamu, uadilifu, weledi na ustawi wa watumishi wa TANAPA vinaendelea kupewa kipaumbele

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara, amesema bodi itaendelea kushirikiana na menejimenti ya shirika hilo kwa kutoa ushauri na miongozo itakayosaidia kufanikisha malengo ya uhifadhi na maendeleo ya utalii nchini.

Aliongeza kuwa uwazi katika uendeshaji wa shughuli za shirika pamoja na utoaji wa mrejesho kwa watumishi wa ngazi mbalimbali ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa

Naye Kamishna wa Uhifadhi, Massana Gibril Mwishawa, amesema ataiongoza TANAPA kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uzalendo, uadilifu na weledi, huku akisisitiza kuwa hifadhi za taifa zina nafasi muhimu katika kulinda bioanuwai, kuchochea uchumi na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mapato yatokanayo na utalii.

Aliongeza kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kushika nafasi hiyo, akiahidi kushirikiana kwa karibu na watumishi wote wa TANAPA ili kuendelea kuimarisha mafanikio ya taasisi hiyo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa taasisi mbalimbali za uhifadhi, akiwemo NCAA, TFS na TAWA, pamoja na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii, viongozi wa dini, maafisa na askari wa TANAPA.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...