Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Serikali imefanikiwa kupata nafasi nyingine 10 za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended, zitakazowawezesha kwenda nchini Urusi kujiandaa na masomo ya shahada katika Chuo Kikuu cha RUDN, Moscow.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma, ambapo amesema nafasi hizo zimetolewa na Chuo Kikuu cha RUDN kufuatia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi mwezi Juni 2026, ambapo alifanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, wanafunzi hao 10 wanatarajiwa kuondoka nchini Septemba 1, 2026 na kuelekea Moscow, ambako watashiriki programu maalum ya maandalizi ya masomo maarufu kama bootcamp kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja, kabla ya kuanza masomo ya shahada rasmi Septemba 2027.

Ameeleza kuwa wakati wa programu hiyo ya maandalizi, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 80 ya gharama, huku asilimia 20 ikigharamiwa kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended. Baada ya wanafunzi hao kuanza masomo yao ya shahada nchini Urusi, Serikali ya Urusi itabeba asilimia 100 ya gharama za masomo yao.

Waziri Mkenda amesema hatua hiyo inaongeza wigo wa fursa za elimu kwa vijana wa Kitanzania, akibainisha kuwa wanafunzi wengine 50 waliopata Samia Scholarship Extended wataenda kusoma nje ya nchi katika maeneo ya Data Science, Artificial Intelligence na Allied Sciences.

Aidha, wanafunzi 1,000 wamepata ufadhili kupitia Samia Scholarship kwa ajili ya kusoma shahada zinazohusiana na sayansi katika vyuo vikuu vya ndani ya Tanzania.

Prof. Mkenda amempongeza na kumshukuru Rais Samia kwa jitihada za kuimarisha mahusiano ya Tanzania na mataifa mbalimbali, akisema nafasi hizo mpya za ufadhili zilizopatikana nchini Urusi zinaonesha mwanzo wa fursa pana zaidi za ushirikiano katika elimu.

Amesema Serikali itaendelea kutumia mahusiano hayo kutafuta fursa zaidi za elimu na ufadhili kwa vijana wa Kitanzania, hususan katika nyanja za sayansi, teknolojia na maeneo mengine yenye umuhimu kwa maendeleo ya taifa.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...