Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Zanzibar

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa rai kwa wananchi wa Kizimkazi na maeneo ya jirani, kuilinda na kuitunza miradi yote ya maendeleo iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi, akisisitiza kuwa ni lazima miradi hiyo itunzwe kama mboni za macho.

Dk.Samia aliyasema hayo leo Agosti 13,2026 katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kizimkazi huko katika kiwanja cha Mgombewa katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni ikiwa ni shamra shamra za Tamasha la Kizimkazi 2026.

Amesema, miradi hiyo mikubwa si mali ya serikali pekee, bali ni uhai, fursa, uchumi na ustawi wa maisha ya wananchi wenyewe na kuongeza Serikali inatumia fedha nyingi pamoja na utaalamu mkubwa kuwaletea wananchi maendeleo hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuzuia uharibifu wa miundombinu hiyo.

“Tutunze itufae leo na litufae tena, tuwe walinzi sisi wenyewe kwa wenyewe, tulindane kutokuharibu miundombinu hii,” amesema Rais Samia na kuongeza kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa maji utaondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa Kizimkazi iliyodumu kwa miongo kadhaa.

Dk.Samia alieleza kuwa tangu mwaka 1974, Kizimkazi ilikuwa ikitegemea tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji.

Ameeeleza kwa miaka iliyofuata mahitaji ya maji yaliongezeka kutokana na kukua kwa idadi ya watu, maendeleo ya makazi, shughuli za kiuchumi pamoja na uwekezaji katika eneo hilo.

Ameongeza tangi hilo ambalo awali lilitosheleza mahitaji ya wananchi, lakini baadae lilichakaa na kushindwa kukidhi mahitaji yaliyokuwa yakiongezeka siku hadi siku.

Dk.Samia amebainisha kuwa hali hiyo ndiyo iliyosababisha changamoto ya maji kuendelea kuwa miongoni mwa kero kubwa kwa wananchi wa Kizimkazi.

“Sasa hali hii imebadilika baada ya kukamilika na kuzinduliwa kwa mradi mpya wa maji wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia wananchi.Mradi huu umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ongezeko la mahitaji ya baadaye.Uwezo wake ukiwa mara mbili ya mahitaji ya sasa ya eneo hilo.”

Ameongeza hatua hiyo haitasaidia Kizimkazi pekee, bali inalenga kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuvuka mipaka na kuwafikia wananchi wa maeneo ya Dimani na Mtende.

Aidha amesema Serikali ina mpango mkubwa zaidi wa kujenga mfumo wa maji wa wilaya nzima, unaojulikana kama district grid, hatua ambayo itapanua zaidi mtandao wa huduma ya maji na kuhakikisha maeneo mengi yanaunganishwa katika mfumo mmoja wa uhakika.

Ameongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo tayari zimepatikana na utekelezaji wake unaanza mara moja.”Kwa Kizimkazi mradi huu haukuwa tu uzinduzi wa miundombinu mipya, bali ni mwanzo wa safari mpya ya huduma ya maji yenye uwezo wa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya eneo hilo.

Aidha amewataka wananchi kuulinda mradi huo na kueleza Serikali imetumia fedha nyingi kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi, hivyo uharibifu wa miundombinu hiyo ni sawa na kuharibu uwekezaji ambao umelenga kuboresha maisha yao wenyewe.

Awali Dk.Samia ametembelea hospital ya Kizimkazi ambapo alipanda mti na kukabidhi gari ya kubebea wagonjwa, ambapo gari hilo limetolewa kwa msaada wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Rais Samia amesema hospitali hiyo sasa imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma, ikiwemo kuanza kutoa huduma ya kusafisha damu, dialysis, kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.

Amesisitiza huduma hiyo ni muhimu kwa sababu kwa kawaida huduma za aina hiyo zimekuwa zikipatikana zaidi katika hospitali kubwa zenye huduma za kibingwa.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...