Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu vijana nchini kwa kuwawezesha kupata mitaji, kulinda haki zao za ubunifu na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali ili bunifu zao ziweze kufikia hatua ya kibiashara na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt Amos Nungu, amesema hayo baada ya kutembelea Banda la Vijana linaloshirikisha washiriki wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kukutana na wabunifu waliopo ndani na nje ya programu hiyo na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Dkt. Nungu amesema COSTECH imeweka mifumo mbalimbali ya kuwawezesha wabunifu, ikiwemo utoaji wa fedha za kukuza bunifu (seed funding), dhamana za mikopo (guarantee schemes) pamoja na kuwaunganisha na taasisi nyingine zinazoweza kuwasaidia kupata mitaji na fursa za kupeleka bidhaa zao sokoni. 

Hata hivyo, amesema bado vijana hao wanakabiliwa na changamoto zinazohusisha usajili wa kampuni, utambulisho wa bidhaa zao na upatikanaji wa vibali mbalimbali, hivyo COSTECH imeanza kushirikiana na wadau husika kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

Amesema kikao hicho kilihusisha pia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Wakala wa Mbolea na taasisi nyingine zinazohusika na sekta ya kilimo na ubunifu, huku akieleza kuwa maoni yaliyotolewa na vijana yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Dkt Nungu, moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni ulinzi wa haki miliki za wabunifu, akisisitiza kuwa ubunifu unapaswa kulindwa ili uweze kuwa na tija kwa mbunifu na taifa kwa ujumla. 

Ametoa mfano wa kijana aliyebuni teknolojia ya kutengeneza mbolea kwa kutumia nywele ambaye, baada ya kupata msaada wa COSTECH katika usajili na ulinzi wa haki zake za ubunifu, aliweza kupata uwekezaji na fedha kutoka nje ya nchi.

“Hii inaonyesha kuwa msaada wa Serikali si fedha pekee, bali pia ni kujenga mazingira rafiki yanayowezesha wabunifu kulinda kazi zao, kuziboresha na kuzifikisha sokoni,” amesema.

Aidha, Dkt Nungu amesema vijana hao wameiomba Serikali kupitia COSTECH kuangalia utaratibu wa marejesho ya mikopo inayotolewa na halmashauri, wakieleza kuwa muda wa kuanza kurejesha mikopo hiyo ni mfupi na hauwapi nafasi ya kutosha kuendeleza miradi yao kabla ya kuanza kulipa. 

Amesema COSTECH imepokea ombi hilo na italijadili kwa kushirikiana na mamlaka husika ili kuona namna bora ya kufanya mazingira ya mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wabunifu na wajasiriamali vijana.

Amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio kwa kuwa kimewezesha Serikali kupata fursa ya kusikiliza changamoto za vijana moja kwa moja na kuweka mikakati ya kuendelea kuimarisha mfumo wa ubunifu, utafiti na teknolojia kwa manufaa ya vijana na maendeleo ya taifa.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...