Na George Maziku, Mbogwe

MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita Pius Lukaga amemsifu na kumpongeza diwani wa kata ya N’homolwa, wilayani Mbogwe, mkoa wa Geita Pili Njile baada ya Diwani huyo kukamilisha ujenzi wa zahanati yake aliyoijenga katika kijiji anachotoka cha Nyanhwiga.

Lukaga ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uzinduzi wa zahanati hiyo iliyopewa jina la PNS, alisema kuwa alichofanya diwani huyo ni utekelezaji Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), 2025-2030 kwa vitendo ambapo ilani hiyo inasisitiza serikali kushirikisha sekta binafsi kuwasogezea karibu wananchi huduma za jamii ikiwemo huduma za afya.

“Huyu Diwani pale wilayani chama tumtambua kama shujaa kutokana na kazi anazofanya za kutekeleza ilani ya chama, tunamshukuru sana kwa kazi anazofanya”, alisema Lukaga.

Aliongeza, “Huyu ni kiongozi mwenye utu na upendo mkubwa, kwasababu alikuwa na uwezo wa kumchukua mme wake kwenda kutalii na kula raha sehemu mbalimbali kama vile Dar es Salaam, Mbeya, lakini aliamua kuwekeza kwenye huduma hii muhimu kwa maisha ya wananchi wake, huu ni upendo mkubwa”, alibainisha kiongozi huyo wa CCM.

Lukaga aliwasihi wananchi wa kata ya N’homolwa kuendelea kumuunga mkono Diwani Njile na kamwe wasimwache kwani viongozi wa aina yake hawapatikani kila mahali na hawapatikani kila wakati.

“Nawaomba sana wananchi wa kata ya N’homolwa msimwache Diwani wenu, mtunzeni sana kama mboni ya jicho kwasababu viongozi wa aina hii hawapatikani kila mahali na hawapatikani wakati wote”, alisisitiza mjumbe huyo wa kamati ya siasa ya wilaya.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, mmiliki wa zahanati ya PNS ambaye pia ni diwani wa kata ya N’homolwa Njile, alieleza huduma zitakazotolewa na zahanati yake kuwa ni huduma za wagonjwa wa nje, upimaji, kliniki ya baba, mama na mtoto, huduma za dharura, na huduma za uzazi wa mpango.

Nae mfamasia wa wilaya ya Mbogwe Salum Mdimu aliyezungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbogwe, aliwahakikishia wananchi wa kata ya N’homolwa kuwa zahanati hiyo imekidhi vigezo vyote vya kisheria vya kutoa huduma za afya kwa watanzania hivyo wasihofu kwenda kutibiwa.

Nao wananchi wa kijiji cha Nyanhwiga waliotoa maoni kwa nyakati tofauti walimpongeza diwani Njile kwa kuwasogezea huduma za afya karibu, na kuwaondolea adha ya kufuata huduma hizo mbali na makazi yao.

“Nimefurahi sana kwa kufunguliwa zahanati hii na diwani wetu ambayo imetupunguzia usumbufu wa kwenda mbali, kabla ya zahanati hii tulisafiri mpaka Masumbwe kwani kuna baadhi ya huduma kama vile za vipimo hazikupatikana kwenye zahanati ya serikali iliyopo hapa kijijini kwetu, lakini sasa tutazipata huduma hizo kwenye zahanati ya diwani ya PNS”, alifafanua Colletha Lenard (31), mkazi wa kijiji cha Nyanhwiga.

“Kwa upande wangu nimefurahi sana kwasababu bado naendelea kuzaa, hii zahanati itakuwa msaada mkubwa kwangu kutokana na maelezo tuliyopewa na diwani wetu kwamba itakuwa na vipimo vyote kwa wazazi, zamani baadhi ya vipimo tulivifuata hospitali za mbali”, alibainisha Agnes Lucas (23), mkazi wa kijiji cha Nyanhwiga.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...