Na George Maziku, Bukombe
VITENDO vya utoroshaji madini nchini kwa sehemu kubwa vinatokana na hatua ya serikali kuweka tozo lukuki kwa wachimbaji, Michuzi Blog imeelezwa.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Chama cha wachimbaji wadogo wilaya ya Bukombe, mkoani Geita (GEREMA), Daniel Lusinge alipozungumza na vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake mjini Ushirombo.
Katika siku za karibuni kuliripotiwa matukio ya watu kukamatwa wakitorosha madini mbalimbali kinyume cha sheria, katika miji mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam ambako pia kuligundulika soko bandia la madini.
Lusinge ambaye pia ni Mwenyekiti wa soko la madini wilaya ya Bukombe aliwaambia wanahabari kuwa wachimbaji wanalipa tozo kuanzia mgodini baada ya kutoa mawe au mchanga kwenye maduara mpaka kwenye hatua ya mwisho wakati madini yanapofikishwa sokoni, jambo ambalo alisema linawakera na kuwakatisha tamaa wachimbaji.
“Ukiacha watu wenye hulka ya kutenda maovu ambao wapo katika kila sekta, utoroshaji wa madini unachangiwa na uwepo wa tozo nyingi kwenye madini ambapo wachimbaji wanaanza kubanwa kwa tozo kuanzia mgodini, kwenye uchenjuaji mpaka sokoni, mambo hayo yanawakera wachimbaji wengi kwasababu wanabeba mzigo mkubwa wa gharama, wanaona kama wanaifanyia kazi serikali, maana watu wote wanataka faida hata serikali yenyewe inataka faida”, alisema Lusinge.
Aliongeza, “Serikali inapaswa kupunguza tozo ili kuwashawishi wachimbaji wasitoroshe madini badala yake waende kuuza kwenye masoko yaliyowekwa na serikali ambayo yapo kila mahali nchini”, alifafanua katibu huyo wa GEREMA.
Kiongozi huyo wa wachimbaji wilayani Bukombe alishauri serikali kuboresha masoko ya madini nchini, huku akishauri utaratibu wa ukusanyaji mapato ya serikali kufanyika soko la madini.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa soko la madini ameishauri serikali kuendelea kuwasaka na kuwaadhibu watu wote wanaojihusisha na biashara haramu ya utoroshaji madini nchini ili kukomesha uhalifu huo na hatimaye kuleta tija kwenye sekta ya madini na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo Lusinge ameiomba serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwaletea mitambo ya utafiti na kuwauzia kwa bei nafuu ili kuwawezesha wachimbaji wengi wadogo kumudu na hatimaye kuchimba kwa uhakika.
“Tunaiomba serikali yetu kuisaidia sekta ya madini kwa kuleta mitambo ya kisasa ya utafiti wa madini ili tuweze kuchimba kwa uhakika. Pia tunaiomba serikali kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya madini ili kukuza sekta na kuifanya kuwa mhimili wa uchumi wa nchi yetu”, alisisitiza Lusinge.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...