Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Jackline Peter, mkazi wa Mji Mdogo wa Katoro, Wilaya na Mkoa wa Geita, kwa tuhuma za kumshambulia kwa fimbo Rahel Jumanne baada ya kumtilia shaka kumwibia fedha.
Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita amesema tukio hilo la kikatili lilitokea tarehe 26 Agosti 2026, saa 5.00 asubuhi nyumbani kwa mtuhumiwa Katoro.
Inadaiwa mtuhumiwa aligundua amepoteza fedha kiasi cha Shilingi 60,000/= zilizokuwa kwenye pochi chumbani kwake. Baada ya hapo alimtilia shaka Rahel Jumanne aliyekuwa amemtembelea kwake.
Kamanda amesema baada ya fedha hizo kudaiwa kupotea, mtuhumiwa alimkamata mwathirika na kuanza kumshambulia kwa fimbo.
Katika tukio hilo, mfanyakazi wa kazi za ndani wa mtuhumiwa alielekezwa kurekodi vitendo hivyo kwa kutumia simu ya mtuhumiwa. Baadaye mtuhumiwa mwenyewe alisambaza picha mjongeo hiyo kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya Jeshi la Polisi kubaini tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, lilifanya ufuatiliaji wa haraka na kufanikiwa kubaini eneo la tukio, kumtambua mtuhumiwa na kumkamata. Kwa sasa anaendelea kuhojiwa.
Kamanda amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mara utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka husika za kisheria kwa hatua zaidi.
Aidha ametoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
"Tuhuma za uhalifu hazimruhusu mtu kutoa adhabu mwenyewe. Mtu anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria ili hatua zichukuliwe," amesisitiza.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...