Na Janeth Raphael – MichuziTv
Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umeendelea kuimarishwa kwa kuunganishwa na zaidi ya mifumo 30 ya taasisi mbalimbali, hatua inayolenga kurahisisha mchakato wa zabuni za umma, kuongeza ufanisi na kuimarisha uhakiki wa taarifa za wazabuni.
Hatua hiyo pia imeongeza uwezo wa Serikali kudhibiti matumizi ya nyaraka zisizo halali katika mchakato wa ununuzi wa umma, huku wazabuni wakipata unafuu wa kuwasilisha taarifa na nyaraka zinazohitajika wakati wa kushiriki zabuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema maboresho hayo yanaendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inaunganishwa na kusomana ili kuwezesha kubadilishana taarifa kwa ufanisi.
Simba ameyasema hayo leo, Agosti 20, 2026, jijini Dodoma wakati akieleza utekelezaji wa bajeti ya PPRA kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2026/2027.
Kwa mujibu wa Simba, NeST kwa sasa imeunganishwa na mifumo zaidi ya 30 inayohusisha maeneo mbalimbali muhimu katika uthibitishaji wa taarifa za wazabuni. Mifumo hiyo inajumuisha mifumo ya kibenki na malipo, hifadhi za jamii, bodi za usajili wa wataalamu pamoja na mifumo inayohusiana na utoaji wa leseni.
Amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kumeboresha kwa kiasi kikubwa namna taarifa za wazabuni zinavyothibitishwa, kwani taarifa muhimu zinaweza kupatikana na kuhakikiwa moja kwa moja kupitia mifumo husika.
Simba amesema hatua hiyo pia imepunguza uwezekano wa kuwasilishwa kwa nyaraka za kughushi katika mfumo wa NeST, kwa kuwa taarifa na nyaraka mbalimbali zinaweza kufanyiwa uhakiki kupitia mifumo iliyounganishwa.
Aidha, amesema mfumo huo umeendelea kupunguza mzigo kwa wazabuni ambao hapo awali walilazimika kuandaa na kuwasilisha rundo la nyaraka katika hatua mbalimbali za mchakato wa zabuni.
“Ndiyo maana tunasema ununuzi wa umma sasa umerahisishwa na unaweza kutumia muda mchache kwa sababu rundo la nyaraka tayari lipo ndani ya mfumo,” amesema Simba.
Amesema matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa umma siyo tu yanalenga kurahisisha taratibu, bali pia kuongeza uwazi, ufanisi na uaminifu katika mchakato mzima wa zabuni.
Kwa hatua hiyo, NeST imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroniki, huku kuunganishwa kwake na mifumo mingine ya Serikali na taasisi mbalimbali kukitarajiwa kuongeza zaidi ufanisi wa huduma na kuimarisha udhibiti wa taarifa katika sekta ya ununuzi wa umma.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...