Wanachama waliohitimu pamoja na familia zao kwenye mahafali ya Awamu ya Pili, Mapigano, Ulyankulu, tarehe 21 Agosti 2026.

Mradi wa DREAMS Tanzania ulianza ukiwa na lengo la kuthibitisha kwamba kaya maskini zaidi zinaweza kujenga biashara zinazodumu. Ndani ya siku nne za mwezi Agosti, kaya 1,356 zilizohitimu zilitoa ushahidi.


ULYANKULU, MKOA WA TABORA, TANZANIA · AGOSTI 2026.

Mwezi Februari 2025, maafisa wa mradi walipita nyumba kwa nyumba katika vijiji vinne vya eneo hili la mkoa wa Tabora. Walikuta kwamba asilimia 14 tu ya kaya maskini zaidi zilikuwa zinaishi kwa zaidi ya dola tatu kwa siku. Baada ya miezi 12 ya utelekelezaji wa mradi, idadi hiyo ilikuwa imefika asilimia 82.75.

Mahafali mawili yaliyotenganishwa na siku tatu yalionesha mabadiliko hayo. Chini ya hema pale Mapigano siku ya Ijumaa tarehe 21 Agosti, kaya 762 kutoka Mbeta, Mapigano na Taba zilipokea vyeti vyao kutoka kwa Jumanne Singani, mkuu wa makazi ya Ulyankulu. Pale Sasu siku ya Jumatatu tarehe 24 Agosti, kaya nyingine 594 zilipokea vyao, huku Mkuu wa Wilaya ya Kaliua akiwa mgeni rasmi. Viongozi wa vikundi walipanda mmoja mmoja kupeana mikono mezani kuu, kuchukua cheti na kusimama kwa ajili ya picha. Kwaya ziliimba, vikundi vya biashara vilitandika mazao, kuku na mchele uliokobolewa, na kila mradi ulipotajwa umati ulijibu jambo lilelile: ongeza kipato cha familia.

Jumanne Singani, mkuu wa makazi ya Ulyankulu na mgeni rasmi, akizungumza na wahitimu kutoka meza kuu pale Mapigano.

Kwa pamoja kaya hizo 1,356 ndio Awamu ya Pili, na zote ziliingia kwenye mradi zikiwa miongoni mwa kaya maskini zaidi ndani ya makazi. Mradi huu unaitwa DREAMS Tanzania, na upo ili kujibu swali ambalo mashirika ya maendeleo yameshughilika nalo kwa miongo mingi: je, familia zilizo kwenye umaskini uliokithiri zinaweza kuingizwa kwenye uchumi wa kudumu, au msaada huishia kupotea tu mara mradi unapoondoka?

DREAMS, au Delivering Resilient Enterprises and Market Systems, unaongozwa na Mercy Corps kwa kushirikiana na Village Enterprise, Caritas Tabora na shirika la msaada wa kisheria la Dignity Kwanza. Utaendelea hadi Desemba 2027, unalenga kujenga uwezo wa kujitegemea kwa watu 150,000 katika makazi ya Ulyankulu, Mishamo na Katumba pamoja na vijiji vinavyozunguka hayo makazi, ambako Watanzania waliopewa uraia na vijiji vinavyowazunguka wanaishi bega kwa bega. Hadi sasa umewafikia watu 140,414.

JINSI MRADI UNAVYOFANYA KAZI

Mbinu yenyewe ni ya polepole kwa makusudi. Hakuna anayekabidhiwa pesa siku ya kwanza. Maafisa hupita kwanza kila kaya katika kijiji kilichochaguliwa wakiwa na dodoso la kupima hali ya umaskini, Poverty Probability Index (PPI), na majibu ndiyo yanayoamua nani anastahili. "Hatukai chini ya mti na mwenyekiti tukamuuliza nani maskini hapa," anasema January Julius Nyanda, anayesimamia timu za uwandani kwa upande wa Caritas Tabora. "Angetutajia majina ya ndugu zake wote."

Katika Awamu ya Pili, kaya 1,670 zilikidhi vigezo na kaya 1,356 zikajiunga. Zilipitia mada tisa za mafunzo kuhusu uendeshaji wa vikundi, elimu ya fedha na ujasiriamali, kisha zikaunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana vya wanachama thelathini hadi arobaini na tano, pamoja na vikundi vya biashara vya kaya tatu tatu. Ndipo pesa ilipofika: shilingi 533,820 kwa kila kikundi, na mgao wa pili wa shilingi 228,720 baada ya miezi sita, jumla ya shilingi milioni 344.4 katika biashara 452.

Kikundi cha biashara kikionesha bidhaa zake kwenye mahafali: miche ya sabuni, sahani zilizopangwa, nyanya na kabichi.

Fredrick Kumbule Modestus, aliyewashauri takribani washiriki 150, anakumbuka waziwazi walipoanzia. "Mtu alikuwa anapata shilingi elfu kumi bila kuwa na wazo kwamba angeweza kutumia elfu saba na kubakiza elfu tatu," anasema. "Wazo la biashara halikuwepo kabisa."

Si kila mtu alijiunga mwanzoni. Zilienea tetesi kwamba mtaji ungerudishwa baadaye, kwa ardhi au kwa mifugo, na baadhi walikaa pembeni mpaka walipoona vikundi vya kwanza vikinufaika.

MWAKA MMOJA UMEZAA NINI

Utafiti wa mwisho, uliofanywa na Caritas Tabora awamu ilipomalizika, ulionesha wastani wa mali za kaya umepanda kutoka dola 260 hadi dola 955, na matumizi kwa kila mtu kutoka dola 164 hadi dola 453. Kaya zinazoweka akiba mara kwa mara zilipanda kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 99.7, na asilimia 91.8 ya biashara zilipimwa kuwa zenye afya wakati wa kuhitimu.

John Brighton Mwangolela ni mkulima wa kitongoji cha Itagwa, kilichoko Sasu. Kwenye mahafali ya Jumatatu alizungumzia mafanikio waliyopata katika kikundi chao;

"Tulianza na mbuzi wanne. Mwisho wa mwaka tukawa na mbuzi kumi na sita. Tukagawana mbuzi mmoja mwenye mimba kila mmoja, na wale kumi na watatu waliobaki tukawauza tukanunua ng'ombe jike mwenye mimba. Hivi ninavyosimama hapa, ana wiki tangu amezaa, na sasa tunakunywa maziwa yake."
John Brighton Mwangolela
Mhitimu, kitongoji cha Itagwa, Sasu

Antonet Yohana ni mwenyekiti wa kikundi cha kuweka akiba cha Muungano kilichoko Taba, ambacho hununua mpunga, hukikoboa na kuuza mchele kwa kupima. Mwezi aliouchagua ni Januari, wakati ada za shule zinapofika na wazazi walipokuwa wanakopa kwa wenye pesa kwa riba aliyoiita nusu kwa nusu. Sasa kikundi chake kinawakopesha wanachama wake wenyewe kwa riba nafuu.

SHERIA ILIBADILISHA NINI

Pesa huleta matatizo yake yenyewe, na ndiyo maana shirika la msaada wa kisheria lipo ndani ya muungano huu wa mashirika. Ulyankulu ni ardhi tengefu na haiwezi kununuliwa wala kuuzwa ndani ya makazi, hivyo kipato kinapopanda ni lazima kiambatane na uelewa wa mahali ambapo ardhi inaweza kununuliwa kihalali. Masala Johnson, afisa wa masuala ya kisheria wa mradi, pia amewasaidia wanachama kupata vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaojiunga na kidato cha tano, na namba za utambulisho wa taifa, ambazo bila hivyo hakuna akaunti ya benki inaweza kufunguliwa.

Timu yake ilifanya kazi kwenye mazingira magumu. "Awali tulipoingia kwenye mradi huu, kulikuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yakiripotiwa ndani ya nyumba, ikiwemo wanaume kutowaruhusu wake zao kuhudhuria mafunzo ya biashara," anasema. "Sasa wapo wanaume wanaotoa ushuhuda kwamba wamewaruhusu wake zao kufanya biashara."

Kwa Mwangolela, masomo ya sheria yalibadilisha namna kijiji chake kinavyozungumzia mabinti.

"Akizaliwa mtoto wa kiume tulisema tumepata mchungaji wa mifugo, na akizaliwa wa kike tulisema tumepata mahari kubwa. DREAMS walitufundisha sheria na wakatufundisha madhara yake. Nenda Itagwa sasa. Shule yetu imejaa watoto kwa sababu ya DREAMS."
John Brighton Mwangolela

MASOKO YENYE SABABU ZAKE ZA KUBAKI

Kinachotofautisha DREAMS na mradi wa kugawa ruzuku ni kinachotokea pale biashara zinapokuwa zimeshaanza. CRDB Bank Foundation ilihamisha pesa kutoka kwenye masanduku na kuiingiza kwenye akaunti takribani 708 katika eneo la Ulyankulu pekee, KickStart International inasambaza pampu za umwagiliaji, SimuSolar inatoa mashine za kusaga na za umwagiliaji zinazotumia nishati ya jua kwa mkopo usio na riba, na AKM Glitters inatoa vifaranga vya siku moja. Mgarang'ombe Traders, wanaokoboa mpunga, walijiunga ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mpunga, nao wakapata kitu.

"Mimi ni mfanyabiashara wa muda mrefu, lakini nilikuwa sina elimu ya biashara. DREAMS walitufundisha, na wakatuomba tuwafikishie wakulima tunaowanunulia mazao. Sasa wanazalisha mchele bora kabisa wa grade A na grade B."
Peter Maganga Mapembe
Wakala, Mgarang'ombe Traders, kata ya Makingi

Kwa mradi mzima, kila dola moja ambayo DREAMS inawekeza imeambatana na dola 4.83 za mtaji wa sekta binafsi.

Kikundi bora cha kuweka akiba katika kila kijiji kilipewa viti hamsini vya plastiki badala ya pesa taslimu, kwa sababu katika vijiji, kila harusi na kila msiba unahitaji viti, viti vinaweza kukodishwa.

KINACHODUMU

Hata zawadi zilibeba mantiki ya mradi. Ili kikundi kistahili kupata viti, kila mwanachama alipaswa kuwa ameweka akiba isiyopungua shilingi 250,000 katika mzunguko wa wiki 52. Pale Sasu zawadi ilikwenda kwa kikundi cha Maboresho, kilichokuwa kimeweka shilingi 12,882,000.

Vyeti vina uzito zaidi. DREAMS hufanya kazi kupitia viongozi wa wilaya badala ya kuwazunguka, na pale Sasu Mkuu wa Wilaya ya Kaliua aliwaambia wahitimu kwamba halmashauri hutenga asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya mikopo ya vikundi, akiwaagiza watumishi wake kuvipa kipaumbele vikundi vyenye vyeti vya DREAMS. "Cheti hicho kimesajiliwa na halmashauri na kinatambulika nayo," Martin Mgallah, meneja msaidizi wa mradi, aliwaambia. "Wenyeviti, kitunzeni. Ndiyo uhai wa kikundi chenu."

Martin Mgallah, meneja msaidizi wa mradi wa DREAMS Tanzania.

Sehemu nyingine za mpangilio wa mradi zinaelekea upande huohuo. Vikundi vya kuweka akiba vinamilikiwa na wanachama wenyewe na havihitaji pesa kutoka nje ili viendelee kufanya kazi, kila biashara ni mali ya kaya tatu badala ya kaya moja, na maafisa wa wilaya wanashikilia kumbukumbu za kila kikundi.

Awamu ya Kwanza ndiyo mtihani halisi wa kwanza. "Tuliwaaga mwaka mmoja uliopita," alisema Mgallah. "Tumetembelea biashara zao jana. Bado wanafanya biashara na wanaendelea kufanikiwa." Mmoja wao ni Abraham Mgaywa wa Makingi, aliyekuwa na familia kubwa na hakuwa na kipato cha kukidhi mahitaji yake wakati dodoso lilipomfikia. Sasa anajiita Mabala the Farmer, na mwezi huu amesafirisha maroli mawili ya matikiti kwenda Dodoma wakati bei ilipokuwa juu kabisa.

Awamu nyingine nne zinaendelea na mafunzo nyuma ya Awamu ya Pili, jumla ya kaya 5,245, na mwakani maafisa watakuwa milangoni Mkindo, Makonge, Kaswa, Usigara, Keza na Ikonongo. Obed Method Bujoro, mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mapigano, anataka warudi kijijini kwake. Ameona jambo ambalo hakuna utafiti ungeliweza kuligundua: watoto wa kaya zenye shida walikuwa wakitokea milangoni kwa majirani wakati wa chakula, na hilo limekoma.

Wahitimu na watumishi wa DREAMS wakicheza mwishoni mwa mahafali.

Anastazia Paulo Makula alisoma risala ya wahitimu pale Sasu. Alijiunga bila mtaji wowote, akajiwekea lengo la kuweka akiba kwa muda wa miezi mitatu, na kwa pesa iliyopatikana akafungua duka la nguo za watoto. Muhtasari wake ndio uliokuwa mfupi kuliko yote siku hiyo.

"Tulikuwa na maisha ya chini sana. Leo nina imani sisi wana Sasu tuko vizuri."
Anastazia Paulo Makula
Kikundi cha kuweka akiba cha Maboresho, Sasu Centre

Mradi wa DREAMS Tanzania unatekelezwa na Mercy Corps kwa kushirikiana na Village Enterprise, Caritas Tabora na Dignity Kwanza, pamoja na wadau wa sekta binafsi wakiwemo CRDB Bank Foundation, Mgarang'ombe Traders, AKM Glitters, SimuSolar na KickStart International.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...