Na Mwandishi Wetu, Mbeya
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 67 wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai katika kipindi cha mwezi Julai 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada zinazoendelea za kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi, wananchi na wadau mbalimbali wa usalama, sambamba na kuendelea kwa oparesheni na misako dhidi ya wahalifu.

Alisema watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo mauaji, kujeruhi, kubaka, kupatikana na silaha bila kibali, dawa za kulevya na wizi. Aliongeza kuwa watuhumiwa ambao upelelezi wa kesi zao umekamilika tayari wamefikishwa mahakamani, huku baadhi yao wakipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo.
Atiwa mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya jirani yake

Miongoni mwa waliokamatwa ni Franko Malaika Green (35), mkazi wa Kibatata wilayani Rungwe, anayekabiliwa na tuhuma za kumuua jirani yake, Edward Nwankusye (38).

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, tukio hilo lilitokea Julai 23, 2026 katika Kijiji cha Kibatata, Kata ya Kisondela, Wilaya ya Rungwe, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumvamia marehemu akiwa njiani kurejea nyumbani na kumkata kwa panga kichwani na mikononi, na kumsababishia majeraha makubwa.

Marehemu alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kwa matibabu, lakini alifariki dunia muda mfupi baadaye.

Kamanda Kuzaga alisema baada ya tukio hilo, kikosi maalumu cha askari wa kuzuia na kupambana na matukio ya mauaji kilianza uchunguzi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani za kishirikina.
Dawa za kulevya, silaha na vipodozi vilivyopigwa marufuku vyakamatwa

Katika oparesheni hizo, Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa saba waliokuwa na kilogramu 12 na gramu 829 za bangi.

Aidha, watuhumiwa watatu walikamatwa wakiwa na lita 17.5 za pombe haramu aina ya gongo, huku watuhumiwa wawili wakinaswa na maboksi 555 ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini. Watu wengine wawili walikamatwa wakiwa na silaha aina ya gobole bila kibali.
Kesi 130 zapata hukumu

Kamanda Kuzaga alisema katika kipindi cha Julai 2026, jumla ya kesi 324 zilifikishwa mahakamani. Kati ya hizo, kesi 130 zilimalizika kwa washitakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo, huku kesi 164 zikiendelea kusikilizwa katika hatua mbalimbali za mahakama.
Madereva wanane wafungiwa leseni

Katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kutoa elimu ya usalama barabarani na kusimamia utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.

Kwa kipindi hicho, madereva wanane walifungiwa leseni zao za udereva baada ya kubainika kufanya makosa hatarishi, ikiwemo kuendesha kwa mwendo kasi na kuyapita magari katika maeneo yenye kona, milima na sehemu ambazo kupita kunakatazwa.
Ulinzi wa Nanenane waimarishwa

Kamanda Kuzaga alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama kuelekea Maonesho ya Nanenane ya Kanda yatakayofanyika mkoani humo.

Alisema doria zimeongezwa katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi na wageni watakaoshiriki maonesho hayo pamoja na watakaotembelea Viwanja vya Maonesho vya John Mwakangale wanakuwa salama.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kushiriki katika elimu za kiusalama ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...